Windows

ZAHERA ACHANA NA SIASA ZA SOKA LA BONGO UFANYE KAZI YAKO




NA SALEH ALLY
NINAAMINI utakuwa umemsikia Kocha Mwinyi Zahera akiwaelezea waandishi wa habari kwamba amepewa taarifa kuwa kuna timu inanunua wachezaji kwa bei ghali na kadhalika lakini imekuwa ikipita huku na kule kutoa fedha ili Yanga ifungwe.

Zahera ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari na msisitizo wake ulikuwa kwamba timu hiyo inatoa fedha kwa timu zinazokwenda kucheza na Yanga.

Kwa mujibu wa Zahera, fedha hizo zinatolewa namna hii; kama timu hiyo itaishinda Yanga basi inapewa milioni 10, ikiitoka sare ni Sh milioni 5.

Kocha huyo Mkongoman akaelezea mifano na kutaja Singida United waliyocheza nayo hivi karibuni na JKT Tanzania pia.

Matokeo ya mecho hizo ilikuwa ni sare na ushindi kwa Yanga. Maana yake katika mechi hizo mbili walipata pointi nne.

Huenda haya yanafanyika kama anavyosema Zahera, lakini kwa kocha tena wa klabu kubwa kama Yanga anapaswa kuwa angalau na uthibitisho.

Amesema kuna wachezaji wa zamani wa Yanga walio katika timu hizo wanawaeleza hali namna ilivyo na walivyopewa hizo bakshishi. Basi ni jambo zuri kwa kuusaidia mpira wa Tanzania kama kitu hicho hakitakuwa sahihi.

Sijaelewa kama watakaokuwa wamefanya hivyo wanaweza kukamatwa kisheria, kwa maana walikuwa wakihamasisha timu fulani ishinde. Kuhamasisha maana yake anayetoa kwa ile timu, atakuwa anaiunga mkono.

Ni sawa na yule anayetoa fedha kwa ajili ya kuisaidia timu anayoipenda ili iifunge timu nyingine. Maana yake anatoa morali kwa kikosi.

Naona kuna tatizo kubwa kwa yule ambaye anamhonga mchezaji wa timu husika, mfano atoe fedha kwa mchezaji wa Yanga, afungishe. Huyu anatoa rushwa.

Tunaweza kuangalia na kujadili lakini onyo langu kwa Zahera, aangalie asijihusishe na siasa za mpira wa Tanzania kupindukia. Kama mtaalamu wa mpira anaweza kujikita katika nafasi yake.

Wakati mwingine anaweza kuwa anajazwa maneno na watu wanaomzunguka kumbe nao wanakuwa hawana uhakika. Mwisho msala utamuangukia yeye atakaposhindwa kuthibitisha.

Pia inawezekana akaanza kujichanganya kama mambo anayoyazungumza yatakosa uhakika na taratibu kuanza kumuonyesha ni mtu anayebahatisha na watu wakachukua hiyo na kuipeleka hadi katika kazi yake ya ufundi ambayo mimi ninaamini ni nzuri.

Anachopaswa kukumbuka Zahera ndani ya Yanga kuna watu wasingependa aendelee kubaki kwa kuwa sijawahi kusikia kuna kocha wa Yanga anapendwa na kila mtu.

Kuna wanaozipenda hizi klabu na wale walio kwa ajili ya maslahi yao na hili ninaweza kulithibitisha kupitia yeye Zahera ambaye aliwahi kusema alidanganywa na kuelezwa baadhi ya wachezaji wangesajiliwa, haikuwa hivyo na mwisho wakasajiliwa ambao hakuwataka kwa kuwa tu tayari dirisha lilishafungwa na hakuwa na ujanja.

Tumesikia mara kadhaa wachezaji katika klabu hizi wakilalama kupunjwa maslahi yao au kuzungushwa kwa kuwa walishindwa kugawana fedha na wahusika wanaofanya usajili. Hivyo suala la watu kuwa ndani ya klabu hizi na wakajali maslahi yao zaidi, si geni.

Msisitizo wangu ni kwa Zahera, aangalie asilishwe maneno yasiyo na ushahidi na yeye akageuka tarumbeta la kuyasukuma kwa jamii, mwisho yatamgeukia na wanaomjaza wao wakakaa kimya, watakaa kando wakimuangalia anavyosumbuka.

Zahera ni kocha wa mpira na anaijua kazi yake. Itakuwa vizuri akajikita katika kikosi chake kwa maana ya ufundi kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri kwa kuwa tayari ameonyesha mwendo bora.

Zaidi pia itakuwa ni kama suala la hamasa kama ambavyo mara kadhaa amefanya, basi angeendelea kuwapa hamasa vijana wake na kuangalia mipango yake sahihi kuliko kurukia ya wengine kwa maneno ya kupewa, mwisho itamuangusha.



Post a Comment

0 Comments