Windows

Ni Prisons Vs Mbeya City leo


Picha
KOCHA wa Tanzania Prisons, Adolf Richard amepania kuondoka na pointi tatu dhidi ya wapinzani wao Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa leo kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.

Prisons inaingia kwenye ‘debi’ hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza kwenye uwanja huo.

Richard alisema mpira ni mchezo wa dakika 90 hivyo watacheza na wapinzani wao kutafuta matokeo chanya kwani kila mmoja kafanya maandalizi yake.

“Tumejipanga, kikosi changu kipo fiti kwa mchezo utakuwa mgumu kwetu sote kutokana na maandalizi kuelekea katika mchezo wenyewe ingawa tulianza kwa kusuasua lakini kwa sasa nadhani mambo yatakuwa mazuri,”amesema Richard.

Mlinda mlango wa timu hiyo, Aron Kalambo amesema morali ya kupata matokeo chanya kikosi hicho kwa sasa ipo juu kutokana na matokeo mazuri waliyoyapata kwenye mechi za hivi karibuni hususani kwenye mchezo kati yao na Azam FC waliowazaba bao 1-0.

Mbeya City kocha msaidizi wa kikosi hicho Mohamed Kijuso amesema licha ya kukabiliwa na changamoto ya kupachika mabao kwa mechi za karibuni baada ya mshambuliaji wao matata Eliud Ambokile kuuzwa nje anaamini kwamba timu hiyo itapata matokeo kwenye mchezo huo.

“Naamini kikosi changu kitafanya vizuri kulingana na maandalizi tuliyoyafanya kama timu, nawaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kutusapoti,” alisema Kijuso. Kwenye msimamo Mbeya City inashika nafasi 11 ikiwa na pointi 30 na Prisons ni ya 15 ikiwa na pointi 29.

Post a Comment

0 Comments