Windows

DKT. KIJAJI AZUIA SH. BILIONI 38 JIJI LA DAR ES SAALAM ILI FEDHA YA AWAMU YA KWANZA IONEKANE THAMANI YAKE

2-min
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akieleza kuhusu uamuzi wa Serikali kuzuia baadhi ya fedha zilizokuwa zipelekwe kwenye miradi ya kimkakati, ili kuhakikisha kiasi kilichotolewa kwa awamu ya kwanza kinafanya kazi iliyokusudiwa, wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku tatu Jijini Dar es Salaam.
3-min
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akielezea jambo wakati wa majumuisho ya ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)  ya kukagua miradi ya maendeleo ambayo imepewa ruzuku na Serikali katika Jiji la Dar es Salaam.
5-min
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Bw. Kisare Makori (kushoto), akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Daniel Chongolo wakati wa majumuisho ya ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Jijini Dar es Salaam
6-min
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Bi. Spora Liana (kulia) na wadau wengine wakifuatilia kwa makini majumuisho ya ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Jijini Dar es Salaam
Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)
………………………
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
SERIKALI KUU imezuia shilingi bilioni 38 zilizokuwa zielekezwe kwenye utekelezaji wa miradi mitatu ya Kimkakati ya kuijengea uwezo wa kimapato Manispaa ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, baada ya kubainika kuwa utekelezaji wa mradi wa Soko la Kisasa la Magomeni uliopatiwa fedha zaidi ya shilingi bilioni 8.5, unasuasua.
Uamuzi huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Dar es Salaam ambapo amekagua miradi kadhaa ya kimkakati iliyopewa ruzuku na Serikali na kubainika kuwa haitekelezwi kwa mujibu wa mikataba.
Miradi mitatu iliyoguswa na uamuzi huo wa Serikali ni Mradi wa uendelezaji wa Ufukwe wa Oyterbay wenye thamani ya shilingi bilioni 14.1, mradi wa Soko la Kisasa la Tandale wenye thamani ya shilingi bilioni 9.7 na mradi wa soko la Kisasa la Kibada wenye thamani ya shilingi bilioni 14, yote ikiwa katika Manispaa hiyo ya Kinondoni.
“Hatutaleta fedha hizi ambazo ni utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya awamu ya pili ambayo Manispaa ya Kinondoni ilipewa ruzuku na mikataba yake kusainiwa mwezi Februari 5, 2019 mpaka hapo tutakapo jiridhisha na utekelezaji wa mradi huo wa Soko la Kisasa la Magomeni kwa sababu watendaji wanaosimamia mradi huo ni wale wale ambao wangesimamia miradi hiyo mipya mitatu” alisema Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji amewataka wakuu wa Wilaya za Ilala, Kinondoni na Ubungo kuhakikisha kuwa wanaisimamia kwa karibu miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo yao ili kutimiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya tano ya Dkt. John Pombe Magufuli, ya kuziwezesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kujitegemea ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Vilevile Dkt. Kiaji ameonya kuwa miradi yote ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa nchini isiingizwe siasa ndani yake kwa kuwa itaharibu maana yake ya kuwa miradi ambayo Serikali imeridhia kuipa fedha ili ianzishwe kwa ajili ya kuchochea maisha na uchumi wa wananchi.
Akiwa ziarani mkoani Dar es Salaam, Dkt. Ashatu Kijaji, alikagua utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambayo ni sehemu ya miradi 22 ya awamu ya kwanza ambayo serikali ilitoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 147 mwezi Mei, 2018, ukiwemo mradi wa soko la kisasa la Kisutu, Soko la Kisasa la Mburahati,  Soko la Kisasa la Magomeni, Ujenzi wa Kituo cha Mabasi Mbezi Louis, na Ujenzi wa machinjio ya Kisasa ya Vingunguti.
Akiwa katika Soko la Kisutu, Dkt. Kijaji alielezea kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa soko hilo na kuutaka uongozi wa Wilaya na Manispaa ya Ilala kungeza kasi ya ujenzi wa soko hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa Wilaya ya  Ilala.
Katika Soko la Magomeni, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amezuia Sh. bilioni 5.5 ambazo zilipaswa kutumika kutekeleza mradi wa Kimkakati wa Soko la Magomeni, liliko wilaya ya Kinondoni, kutokana na kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mradi huo licha ya kupewa sh. bilioni 3 za kianzio miezi kadhaa iliyopita lakini utekelezaji wake unasuasua.
Akiwa katika Soko la Kisasa la Vingunguti, ameinyang’anya Manispaa ya Ilala, mkoani Dar es Salaam shilingi bilioni 3 ilizoipatia kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kimkakati wa Machinjio ya Kisasa wa Vingunguti, baada ya Manispaa hiyo kushindwa kuanza kutekeleza mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 8.5.
Dkt. Kijaji pia alitembelea ujenzi wa Mradi wa Kituo Kikuu kipya cha Mabasi yaendayo ndani na nje ya nchi cha Mbezi Louis ambacho ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 50.9 na kuelezea kuridhishwa kwa kiasi fulani na utekelezaji wake lakini akautaka uongozi wa Wilaya ya Ubungo kuongeza kasi ya ujenzi huo ambao kukamilika kwake kutaliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuingiza mapato ya zaidi ya sh. bilioni 7 kwa mwaka.
Akiwa katika Soko la Mburahati, Wilaya ya Ubungo, Dkt. Kijaji alionya kuhusu mabadiliko yoyote ya michoro ama usanifu wa mradi huo unaotekelezwa kwa ubia kati ya Sekta Binafsi na Serikali wenye thamani ya shilingi bilioni 2 ambapo Serikali imetoa zaidi shilingi milioni 900, kwamba usije ukaongeza gharama za ujenzi kwa sababu Serikali haiko tayari kutoa fedha za nyongeza.

Post a Comment

0 Comments