KAJA Mwarabu tena na kikosi chake na mabilioni, akakaa! Akafuata Yanga mwenye Heritier Makambo, naye akakaa.
Sembuse Azam inayotokea kule Mbagala ndanindani? Meddie Kagere ni mtu mbaya sana. Wakati Simba wakishangilia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Azam FC, mshambuliaji wao John Bocco alikuwa akijiwekea rekodi ya aina yake kikosini humo.
Simba jana ilikuwa mgeni wa Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ikiwa ni mechi yao ya kwanza msimu huu katika ligi kuu timu hizo kukutana.
Bocco ambaye alijiunga na Simba, msimu uliopita, mpaka sasa amefunga mabao saba kwenye ligi kuu, lakini kama hujui alikaa kwa takribani miezi mitatu bila ya kufunga, lakini alipoanza kufunga, hivi sasa amekuwa akitupia tu au kutoa asisti.
Rekodi hiyo inaonekana kutisha ndani ya Simba akishirikiana vyema na mshambuliaji Meddie Kagere ambaye ana rekodi ya kufunga pia kwenye mechi kubwa tangu atue Simba msimu huu. Kagere alifunga kwenye mechi dhidi ya Al Ahly bao moja, Yanga (1) na jana mbele ya Azam (2).
Kuanzia kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Bocco alianza kufanya mavituzi baada ya kumpa pande zuri mshambuliaji Kagere na kufanikiwa kuichapa Al Ahly kwa
bao hilo pekee ukiwa ni ushindi wa pili kwenye kundi lao.
Baada ya hapo, Bocco akaanza kutiririka na asisti kwani alitoa nyingine kwenye mechi iliyofuatia dhidi ya watani zao Yanga ambao walikufa bao 1-0, mfungaji akiwa ni yuleyule Kagere raia wa Rwanda.
Pacha yao inaonekana kuzaa matunda zaidi kwani, licha ya Kagere kutosafiri na Simba Jumanne iliyopita kwenda Arusha kucheza na African Lyon, Bocco hakuonyesha kutetereka kwani alifanikiwa kufunga mabao mawili huku akisababisha bao lingine la tatu kwa Adam Salamba, huko Simba ilishinda mabao 3-0.
Wakati Bocco akifanya hayo Arusha, Kagere alikuwa ametulia kwenye sofa akimuangalia vyema pacha wake na namna ya kuendelea kuzitumia pasi ambazo angekuwa akimtengenezea.
Hapo kumbuka kituo kilichokuwa kikifuata ni Azam. Fowadi ya Simba chini ya Emmanuel Okwi, Kagere na Bocco ilionekana kukamia mchezo huo wa jana ambao Clatous Chama na Jonas Mkude walipaka rangi sana katika sehemu ya kiungo ya Simba.
Kwa kimo Bocco ni mrefu zaidi ya Kagere lakini wamekuwa wakipimiana vyema mipira, sasa jana hiyo dhidi ya Azam, kasi yao iliendelea kutisha kama kawaida.
Kutokana na kusomana vilivyo, Bocco jana alipiga mpira ambao uligonga mwamba na kurejea uwanjani lakini kabla mabeki wa Azam FC hawajaokoa, Kagere asiyependa kukata tamaa aliibuka na kuusukumiza mpira kimiani na kumuacha kipa Razack Abalora akiwa hana la kufanya dakika ya nne.
Wakati Azam wakijiuliza nini kimetokea, dakika ya 38, Bocco alitumia vyema krosi ya nje ya 18 iliyopigwa na Zana Coulibaly ambaye usajili wake ulibezwa sana na mashabiki wa Yanga. Nahodha huyo wa Simba ambaye ni mchezaji wa zamani wa Azam, hakushangilia sana bao hilo kama ishara ya uungwana wa kimchezo wa timu hiyo ambayo ilimkuza kisoka.
Kwa hasira, kipindi cha pili kabla hakijaanza, Azam ikawatoa Ramadhan Singano na Tafadzwa Kutinyu, nafasi zao zikachukuliwa na Enock Agyei na Donald Ngoma. Kagere jana alifikisha bao lake la 11 na kuzidi kumvuta Makambo ambaye ana mabao 12.
Kipindi cha pili mastaa wa Azam, Mudathir Yahya, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ na Obrey Chirwa, waliwachachafya vilivyo Simba na kutengeneza nafasi kadhaa za wazi ambazo nyingi walikosa maarifa ya kuzitumia.
Kocha wa Azam, Hans Pluijm na wasaidizi wake, muda mwingi walionekana kuishiwa mate kwani walikuwa wakishangaa ni nini kimewakumba wachezaji wao ambao walikuwa na morali kubwa kambini na hata wakati wanapasha kuanza mchezo huo.
Awali, Pluijm ambaye msimu huu amenunua mastaa wengi wazoefu, kabla ya mchezo huo alijinasibu kwamba dawa pekee ya kubeba ubingwa wa msimu huu ni kuzizuia Simba na Yanga, ingawa jana mtihani wa kwanza aliushindwa na kufanya mabosi wake waanze kukuna vichwa.
Kama hiyo haitoshi, yuleyule Kagere aliiandikia bao la tatu Simba akiunganisha pasi nzuri ya Mzamiru Yassin dakika ya 77 ambapo alimlamba chenga beki wa Azam na kuachia shuti ambalo lilimshinda kipa Abalora. Azam nao walikuja juu na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Frank Domayo kwa shuti kali ndani ya 18 dakika ya 81.
Simba ilimaliza mchezo huo kwa kupata pigo kutokana na mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi kuumia dakika ya 67 baada ya kugongana na beki wa Azam, Bruce Kangwa. Okwi alishindwa kuendelea na mchezo huo na alionekana akivuja damu kwenye paji la uso. Nafasi yake ikachukuliwa na Mzamiru Yasin.
Hata hivyo Daktari wa Simba, Yassin Gembe, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kusema Okwi yuko poa na atacheza mechi inayofuata dhidi ya Lipuli.
Vikosi vilivyoanza; Azam: Razak Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Tafadzwa Kutinyu, Obrey Chirwa na Ramadhani Singano. Simba: Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.
0 Comments