Simba, juzi ilijikuta ikichezea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa AS Vita katika mchezo wa pili wa Kundi D kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs de la Pentecôte huko Congo.
Huo ni mchezo wa pili wa Simba kucheza katika michuano hiyo baada ya ule wa awali dhidi ya JS Saoura kupata ushindi wa mabao 3-0 jijini Dar es Salaam.
Zahera alisema aliiona Simba inacheza mchezo huo kama inacheza mechi ya kirafiki na siyo Ligi ya Mabingwa Afrika kama walivyocheza AS Vita.
Zahera alisema, wachezaji wa timu hiyo walishindwa kutimiza majukumu yao ya ndani ya uwanja kwa kuanzia mabeki na viungo ambao walionekana kutegeana katika ukabaji katika eneo la katikati na golini kwao.
“Kwa mara ya kwanza niliiona Simba ikicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama inacheza mechi ya kirafiki, wakati ilipocheza na AS Vita, kiukweli nilishangaa kuiona Simba hii ninayoijua mimi.
“Wachezaji wake walionekana kama hawapo uwanjani vile na hakukuwa na muunganiko mzuri kati ya safu ya kiungo na ushambuliaji katika kulishambulia goli la AS Vita.
“Simba hawakucheza mpira kabisa katikati zaidi walikuwa wanaonekana wachezaji wa pembeni, mabeki na mawinga na siyo viungo wa katikati na hilo lilikuwa wazi, wachezaji wenyewe walionekana kutoumizwa na mabao waliyokuwa wanafungwa, hilo lilionekana wakati mpira unaingia wavuni wenyewe, walionekana kuinama na kushika viungo na hata sura zilikuwa hazionekani kukasirika,” alisema Zahera.
0 Comments