Ajibu amewaangalia mastraika hao pamoja na wengine wanaokimbizana kwenye mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora msimu huu na kuamua kujiengua akiwaachia wenzake, lakini akimpa moja kwa moja Makambo kuwa lazima msimu huu abebe tuzo hiyo.
Makambo ndiye kinara kwa sasa akiwa na mabao 11 akifuatiwa na Eliud Ambokile wa Mbeya City na Said Dilunga wa Ruvu Shooting wakiwa na mabao 10 kila mmoja huku Kagere na Emmanuel Okwi wa Simba wakiwa na mabao saba kila moja kama Dickson Ambundo wa Alliance, Emmanuel Mvuyekure wa KMC, Vitalis Mayanga wa Ndanda, nyuma ya Salum Aiyee mwenye mabao tisa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ajibu ambaye kwa sasa ndiye nahodha wa Yanga, alisema kazi yake kubwa ndani ya Yanga ni kuhakikisha anatengeza nafasi nyingi za mabao kwa wenzake na ikitokea anakuwa kwenye nafasi ya kufunga, basi atafanya hivyo.
“Sitaki uchoyo wa kung’ang’ania kuzifumania nyavu pale ninapoona siwezi kufanya hivyo, ndio maana nimeamua kujiondoa kwenye mbio hizo za Mfungaji Bora na kuwaachia wengine, ila Makambo ndiye atakayebeba kwani jamaa anajua kufunga,” alisema.
“Lengo langu kubwa ni kuona Yanga inaandika rekodi ya aina yake, kuhakikisha tunamaliza msimu kishujaa na sio mchezaji mmoja mmoja kupata sifa ambazo hazitakuwa na manufaa ya klabu,” alisema Ajibu aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Simba.
Mbali na hilo, Ajibu pia alizungumzia namna Yanga inavyoweza kutwaa ubingwa kwa msimu huu kwani hawajakurupuka, bali ni mpango wao tangu ligi ilivyoanza.
Alisema wana kila sababu ya kutwaa ubingwa kutokana na kuwa katika nafasi nzuri na matokeo mabaya waliyoyapata katika mchezo ulioisha wameyasahau wanaangalia mchezo mwingine uliombele yao.
“Hakuna siku tulitamka kuwa hatuwezi kufungwa, hivyo matokeo tuliyoyapata tumeyapokea, tulitengeneza nafasi nyingi lakin tulishindwa kuzitumia wenzetu waliipata moja wakaitumia mapambano bado yanaendelea lengo ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa ligi,” alisema Ajibu.
Aliongeza kupoteza kwao mchezo dhidi ya Stand United mjini Shinyanga imewafanya wachezaji wa Yanga kutambua wapi wamekosea na kujisahihisha, huku akisisitiza anaamini kocha wao, ameyaona makosa waliyoyafanya na watayafanyia kazi kabla hawajaingia uwanjani kukutana na timu nyingine na kuweka wazi kuwa kikubwa walichonacho wao kama wachezaji sio kuridhika.
“Tunaongoza ligi kwa pointi nyingi sana, wanaotufuata nyuma yetu wana viporo wakishinda wanaweza kutufukuzia na kutufikia, hivyo tunatakiwa kupambana zaidi kutengeneza pointi na idadi kubwa ya mabao ambayo yanaweza kutubeba mwisho wa msimu,” alisema fundi huyo wa mpira ambaye amekuwa akitoa asisti nyingi kwa wenzake.
0 Comments