Wachezaji wa Yanga, wamepewa mamilioni ya fedha licha ya kuchezea kichapo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi Stand United juzi Jumamosi.
Kwa mara ya kwanza katika michuano ya ligi kuu msimu huu, Yanga ilikubali kupoteza mchezo wake baada ya kutandikwa na Stand United bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Yanga ilikumbana na balaa hilo baada ya kucheza mechi 19 bila kufungwa lakini mechi yake ya 20 ikakumbana na balaa hilo.
Hata hivyo, mara baada ya mechi hiyo baadhi ya wadau wa klabu hiyo, waliwakabidhi wachezaji wa Yanga Sh 2,000,000 baada ya kuvutiwa na uwezo waliouonyesha licha ya kufungwa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema: “Ni kweli kabisa wachezaji walipewa fedha hizo kutoka kwa wadau hao kwa ajili ya kuwapongeza pia kuwapa moyo licha ya kufungwa.
“Lakini pia kuna mdau mwingine pia aliwaahidi kuwapatia fedha nyingine kwa ajili ya kuwapa moyo, hakika ni jambo zuri na litazidi kuwapa morali wachezaji kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zetu zijazo.
“Matokeo ya mechi hiyo tumeyapokea japokuwa kulikuwa na upungufu wa hapa na pale kutoka kwa waamuzi, lakini imeshatokea inatubidi tujipange kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zijazo.”
0 Comments