Windows

Vifaa vipya Simba vyakataliwa

KINACHOENDELEA huko Simba ni vurugu tupu unaambiwa kwani, wale wachezaji waliotua kwa majaribio Hunlede Kissimbo, raia wa Togo na beki Lamine Moro kutoka Ghana, wamezusha kizaazaa cha kutosha.
Wachezaji hao walitua nchini wiki iliyopita kwa ajili ya kufanya majaribio ili kuangalia kama wanaweza kulamba dili la kukipiga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, lakini wadau wa soka wakiwemo makocha na wachambuzi wamewakataa mchana kweupee.
Juzi Jumatano wakati Simba ikiichapa AFC Leopards (Ingwe) mabao 2-1, wachezaji hao walianza kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Patrick Aussems, lakini viwango walivyoonyesha ndio vikawaibua makocha.
Kissimbo, ambaye ni mshambuliaji alianza sambamba na Emmanuel Okwi lakini kila Mganda huyo alipowapangua mabeki wa Ingwe na kumpigia krosi nzuri straika huyo Mtogo  zilimpita na kushindwa kutumbukiza mpira wavuni. Baada ya kipindi cha kwanza mchezaji huyo alitolewa na nafasi yake kuingia Meddie Kagere.
Kwa upande wa beki Lamine Moro yeye alipata ahueni kwani, alianza kucheza na Pascal Wawa na baadae alicheza na Juuko Murushid ingawa alionekana mzito na kufanya makosa kadhaa yaliyozimwa na wenzake.
Simba hawakuishia hapo kwani siku hiyo hiyo baada ya mechi timu hiyo ilishusha mchezaji mwingine raia wa Namibia, Sadney Urikhob ambaye naye amekuja kwa majaribio.

Wasikie hawa makocha
Kocha wa Prisons ya Mbeya, Mohammed Adolph Rishard, amesema wachezaji hao wawili wa kigeni ni wa kawaida sana na atashangaa kama watasajiliwa na Simba.
Rishard, ambaye alikuwepo uwanjani katika mchezo huo alisema wachezaji hao walionyesha kiwango cha kawaida na wala hawana sifa za kuitwa wa kimataifa.
“Sijui kama wamewasajili au ndio wako katika majaribio, lakini hawana kiwango cha kucheza Simba kwani ni wa kawaida sana.
“Tukianza na yule beki alikuwa akifanya makosa mengi ambayo Wawa na Juuko waliyafuta na cha kushukuru AFC Leopards hawakuwa na kasi, lakini yule mshambuliaji ndio alikuwa ovyo kabisa kwani, alishindwa kwenda na kasi ya wenzake na anaonekana mzito,” alisema.
Naye Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Mshindo Msola amewashangaa Simba kuleta wachezaji wa majaribio na kusema hakutegemea hayo yatokee tena.
“Hivi mchezaji mzuri anafanyiwa majaribio?. Wanashindwa kujifunza kwa wenzetu Ulaya, wakimtaka mchezaji kwanza wanamfuatilia halafu anasaini, anapimwa afya na mambo mengine yanasonga kwa nini hapa tunashindwa na kufanya mambo kwa mazoezi. alisema Msola.
Kwa upande wake kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema anashangazwa kuona wachezaji wanatoka nje ya nchi, lakini wakizidiwa viwango hata na wachezaji wa ndani.
“Wale wachezaji hawana viwango yule mshambuliaji ndio kabisa labda kidogo beki  alionyesha uhai ingawa huwezi kusema ana kitu cha ziada mguuni kwake.

Aussems naye afunguka
Wakati wataalamu hao wa soka wakiponda viwango vya wachezaji hao, Aussems wala hana haraka na ndio kwanza amesema atawapa muda zaidi kabla ya kufanya uamuzi.
“Bado wanahitaji muda zaidi na kuwaangalia katika mechi nyingne ili kuona kama wanastahili kusajiliwa ndani ya kikosi hiki,” alisema Aussems.

Simba ya Mo Dewji
Wakati Simba ikiachana na mfumo wa zamani na kuingia mpya, aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah’ Try Again alikaririwa akisema kuwa kuanzia sasa Simba itakuwa makini kwenye usajili sio kufanya mambo yasikuwa kwenye mpango.

Post a Comment

0 Comments