N I wakati mwingine mzuri tunapokutana jamvini kujadili mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Wiki iliyopita tulianza kujadili kuhusu mada hii kama inavyojieleza hapo juu. Narudia kukusisitiza, furaha ya kweli ndani ya moyo wako, ya maisha na hasa mapenzi, inaanzia kwako. Ni makosa makubwa kumtegemea mtu mwingine ndiyo akamilishe furaha yako kwa sababu ikitokea akashindwa kufanya hivyo, madhara yake ni makubwa. Yawezekana unampenda sana mwanaume uliyenaye, au yawezekana unampenda sana mwanamke uliyenaye lakini unapaswa kujua kwamba inawezekana siku akakuumiza sana moyo wako.
Ukielewa hilo, utakaa kwa tahadhari, hata kama unampenda sana bado utaitambua thamani yako. Ni mpaka pale unapoweza kujipenda wewe kwanza, ndipo unapoweza kuwa na amani na furaha ya kweli katika maisha yako.
Acha kujidanganya kwamba bila yeye huwezi kuishi kwa sababu inawezekana kweli leo anakupenda sana lakini huwezi kujua kesho yako ikoje, akili za binadamu zinabadilika mara kwa mara. Kwa hiyo, kama ulikuwa umejisahau, ni wakati wako sasa wa kuanza kujipenda mwenyewe kwanza. Ni rahisi, na inaanzia katika akili yako. Jiambie kwamba wewe ni mtu wa kipekee na hakuna mtu mwingine kama wewe na hatatokea.
Jiambie kwamba thamani uliyonayo leo hii, haitokani na mtu uliyenaye kwenye mapenzi, bali ni kwa sababu ulizaliwa ukiwa na thamani yako. Jiwekee malengo ya peke yako katika maisha, na hapa simaanishi kwamba uanze kujitenga na umpendaye na kujifanyia mambo peke yako. Mnapokuwa mnapendana, mnakuwa na malengo mengi ya pamoja na mara nyingi haya ndiyo yanayowaumiza sana watu inapotokea mmeachana. Mnaweza kuwa na malengo ya pamoja lakini pia unapaswa kuwa na malengo binafsi, iwe ni katika kazi, katikamaisha binafsi, katika elimu na kadhalika.
Tenga muda wa kuwa peke yako! Unajua mkiwa kwenye mapenzi, unakuwa unatamani sana upate muda wa kuwa na yule umpendaye. Hiyo ni sawa lakini huwa unakumbuka kupata muda wa kuwa peke yako? Siyo kwa lengo baya, unaweza hata kuamua kutoka peke yako, au kukaa mahali na kutafakari kuhusu maisha yako ukiwa peke yako. Yatazame maisha yako kuanzia ulikotoka, ulipo na unapotaka kufika, mambo uliyoyapitia, changamoto, mafanikio, furaha na huzuni pia.
Ukijenga utaratibu huu, utaanza kuijua thamani yako mapema na ujasiri wa kukabiliana na maisha yako utaongezeka. Pia dumisha uhusiano mzuri na watu wanaokuzunguka, au wenye msaada kwenye maisha yako. Yawezekana pengine baada ya kukutana na huyo uliyenaye, uliamua kubadilisha kabisa aina ya marafiki ulionao.
Hilo siyo jambo baya lakini unapaswa kuelewa kwamba kuna maisha nje ya mapenzi, na watu wako wa karibu ndiyo wanaoweza kuwa msaada mkubwa kwako endapo mambo yataenda ndivyo sivyo, kwa hiyo ni muhimu kuwa na uhusiano mzuri na ndugu, jamaa na marafiki ingawa hawatakiwi kukuchagua jinsi ya kuishi na mwenzi wako.
Zingatia afya yako, hakikisha unakula vizuri, unafanya mazoezi na unapata muda wa kutosha wa kupumzika. Linda mwonekano wako, kwa sababu wapo ambao baada ya kuingia kwenye uhusiano, hujiachia na kunenepeana kwa sababu ya kuridhika na kupoteza mvuto.
Jipende, linda mwonekano wako, vaa vizuri, jipende na jiamini. Ukizingatia haya, hata ikitokea amekutenda, utakuwa na nafasi nzuri ya kukabiliana na maumivu kwa sababu tayari ulishasimama kwenye misingi yako kabla hata hajaondoka.
0 Comments