Walimu 12 waliokuwa wanafundisha katika Shule ya Sekondari Masjid Qubah Muslim Seminary jijini Dar es Salaam wanatarajia kufukuzwa na kuajiriwa wapya kutokana na shule hiyo kuwa ya mwisho kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.
Katika matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa jana jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, shule hiyo iliyoko Kijitonyama jijini imefunga orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya zaidi.
Shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 43 waliandikishwa kufanya mtihani huo, lakini wawili (mvulana na msichana) hawakuufanya.
Kati ya wanafunzi 41 (wavulana 27) wa shule hiyo waliofanya mtihani huo na kuipa matokeo hayo mabaya, 15 wamepata daraja la IV na 26 wamepata daraja 0, hivyo shule yao haina ufaulu wa daraja I-III.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Abubakar Musa, amesema kuwa matokeo hayo yamesababishwa na uongozi mbaya uliopita. Alidai kupewa uongozi Desemba 28, mwaka jana, baada ya wanafunzi hao kufanya mtihani huo.
"Tulianza kuisafisha shule kwa kumwondoa mkuu wa shule kwa sababu hali haikuwa nzuri na matokeo ndio kama yanavyoonekana, watoto wamefeli wote. Walimu hawa 12 tuliwaambia tutawapima kutokana na ufaulu wa wanafunzi, kwa matokeo haya wote tunawafukuza," alisema.
Mkurugenzi huyo alisema walikaa kikao jana na kingine cha menejimenti kitakaa tena ili kuwaondoa walimu hao.
0 Comments