NA SALEH ALLY
LAZIMA utakuwa unakumbuka utawala usioisha nguvu wa Waarabu katika soka la Afrika. Hakika jamaa wanajua mpira lakini waliendesha maisha yao kwa fitna sana.
Kwa wale waliobahatika kuhudhuria mechi za soka katika nchi za Kaskazini mwa Afrika wanajua namna mambo yanavyokuwa.
Hakika Waarabu walikuwa wanafanya wanavyotaka wao hasa kwa timu zinazotoka Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mashabiki wao walikuwa wakionyesha dharau ya kupindukia na ilikuwa hakuna namna ya kuwafanya zaidi ya kungalia kila jambo bila ya kuwazidi.
Ajabu zaidi hata pale walipotoka nje ya nchi zao kwa ajili ya mechi kadhaa, walionyesha dharau kubwa kwa mashirikisho ya nchi husika.
Wachezaji wao walikuwa wababe wasiokuwa na woga hata kidogo. Lakini mambo sasa ni tofauti kabisa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), si lile lililozoeleka.
Caf ya sasa ni tofauti kabisa na ile ya zamani licha ya kwamba makao makuu yake yanaendelea kuwa Cairo, lakini timu inayokosea, basi hatua zinachukuliwa.
Haki ya uhakika wakati huo isingeweza kuwa kwa kiwango cha juu kwa nchi za Kaskazini kama Misri, Algeria, Tunisia, Libya. Lakini sasa, Caf wao haki ni haki bado.
Caf wametoa adhabu kwa Klabu ya Ismaily ya Misri, wameiondoa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tena hatua ya makundi. Waswahili wanasema ukiona mwenzako ananyolewa…
Ismaily imekutana na rungu hilo baada ya mashabiki wake kusababisha mchezo kumalizika kabla ya muda wake dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Mashabiki hao walimshambulia mwamuzi wa akiba pamoja na benchi la Club Africain, mwamuzi akamaliza mchezo. Awali, wangeweza kunyang’anywa pointi tatu tu. Lakini sasa, mambo ni tofauti, wametolewa na hii ni hasara kubwa kwao.
Hili si jambo dogo, wala si jambo la kuliacha lipite tukiona ni kama mzaha badala yake kuna kila sababu ya kulichukulia kama tahadhari kwetu pia.
Nasema ni tahadhari kwa kuwa Tanzania ndio nchi pekee ukanda wa Afrika Mashariki wenye timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Simba ndiyo wako katika hatua hiyo na tunajua kwamba watacheza mechi mbili zilizobaki za Kundi D kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Suala la nidhamu ya mashabiki linapaswa kuwa juu katika kiwango kinachohusisha usikivu wa juu kabisa.
Nasema hivyo kwa kuwa kama mashabiki watajisahau na kuendelea na matukio kadhaa ambayo tumeyaona katika mechi za Ligi Kuu Bara au Kombe la Shirikisho, basi Simba iko hatarini.
Kama leo Caf inaonyesha haina utani hata na timu za Misri, maana yake yeyote sasa anaweza kuchukuliwa hatua na hakutakuwa na nafasi ya kupindisha sheria.
Hakuna ubishi kwamba mashabiki wa Ismaily watakuwa wanajuta kwa kuwa wamepoteza heshima, faida na burudani kwao.
Wao hawatapata nafasi ya kuziona mechi nyingine kwenye uwanja wao timu yao ikipambana. Hii ni burudani ambayo bila shaka waliitaka kwa nguvu zote.
Wamepoteza heshima ya klabu yao kupitia timu yao kuwa katika hatua hiyo muhimu sana. Lakini faida kwa wachezaji na klabu kwa ujumla.
Klabu inatumia michuano kujiingizia fedha kupitia mashabiki. Inaweza kujitangaza na kuwatangaza wachezaji wake kwa ajili ya soko la kuwauza.
Kumbuka klabu inaingiza fedha kwa viingilio, haki za runinga lakini pia kuwaridhisha na kuwashawishi zaidi wadhamini.
Hivyo, mashabiki wa Simba lazima wajue kama itatokea mwamuzi amekosea, wasithubutu kuiadhibu Simba kwa kisingizio cha kosa la mwamuzi, Caf haitakuwa na muda wa maelezo.
0 Comments