N I Jumatatu nyingine ambayo Mwenyezi Mungu ametukirimia pumzi yake. Tumshukuru kwa hilo. Karibu jamvini mdau. Mada hapo juu ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na wengi katika kipindi tulichonacho. Ukweli ni kwamba kumekuwa na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuwaje vijana wa kiume wamekuwa hawaoi?
Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume wanaoogopa kuoa inavyoongezeka. Utakuta wapenzi wanaambiana wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga.
KWA NINI?
Hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo hili, lakini yapo mambo ambayo yanaweza kutupa angalau tafakuri;
UKOSEFU WA MTU WA MFANO
Hapa nawazungumzia wale watoto wa kiume waliolelewa na upande mmoja yaani mama peke yao. Sina maana ya kudharau malezi ya mama, lakini ni vyema mkafahamu kwamba kuwa na baba asiye na malezimazuri si sawa na kutokuwa na baba kabisa. Na ndiyo maana nikasema ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano (role model).
Achilia mbali aina ya malezi atakayoyapata mtoto, yawe mazuri au mabaya, lakini lazima kutakuwa na tabia za kiume zitakazoakisi malezi ya mtoto wa kiume. Watoto waliolelewa na mama peke yao kuna kitu wanakosa, kwani wanakuwa hawana mtu wa kumchukulia kama mfano kwa upande wa jinsi ya kiume na hapo ndipo hujikuta wakijifunza wenyewe namna ya kuongea na kutenda kama wanaume kwa sababu katika makuzi yao hawakupata fursa ya kuwa karibu na baba zao.
Kwa kuwa siku hizi kuna kundi kubwa la akina mama ambao wamejikuta wakiachiwa mzigo wa malezi ya watoto, baada ya kuachwa na waume zao au kuzalishwa na kutelekezwa (single mothers) na hapo ndipo tunaposhuhudia mtoto wa kiume anapokua kwa umri na kimo huku akiwa hana mtu wa kumuangalia kama mfano wa
mume anavyotakiwa kuwa katika familia zaidi ya kujifunza mambo hayo kupitia katika runinga, sinema au muziki.
Wanaume waliopitia malezi ya aina hii huchelewa sana kuoa kwani huyaangalia maisha ya ndoa kwa namna ya kujaribu na ndipo hapo wengi huishia kuishi kinyumba na wanawake kwa ajili ya kutaka kujifunza namna ya maisha ya ndoa yanavyotakiwa kuwa na ndiyo sababu huchukua muda mrefu kufanya uamuzi wa kuoa. Na mara nyingi huishia kubadili wanawake.
MGOGORO WA KIUCHUMI
Kuna kundi kubwa la vijana siku hizi hawana ajira au hawana uhakika na kipato. Ukweli ni kwamba hakuna mwanaume atakayependa kujiingiza kwenye ndoa wakati hana kazi au hana uhakika na kipato chake. Na hiyo ni kutokana na wanawake wengi siku hizi kuonekana kujali zaidi wanaume wenye uhakika na kipato. Hii misemo ya wanawake ya kebehi kwa wanaume wasio na ajira au kipato, kama vile mwanaume suruali ina mchango mkubwa sana katika kuwafanya wanaume kukwepa kuoa iwapo hawana uhakika wa kipato.
WANAWAKE KUWA NA ELIMU YA JUU
Siku hizi wanawake wengi wameibuka katika kutafuta elimu ya juu kwa juhudi kubwa. Idadi ya wanawake wanaojiunga na vyuo vikuu ni wengi tofauti na ilivyokuwa zamani. Na hiyo ni kutokana na wazazi wengi kubadili mtazamo wao juu ya mtoto wa kike.
Zamani mtoto wa kike alichukuliwa kama kitega uchumi. Kwa maeneo ya vijijini na katika familia maskini, watoto wa kike walikuwa wanatazamwa kama biashara ya kesho ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ilikuwa ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na siyo kibinadamu. Lakini tofauti na zamani, siku hizi hata kule vijijini kumekuwa na mwamko mkubwa wa kumsomesha mtoto wa kike hadi elimu ya juu.
Kutokana na mwamko huo wanawake wengi wamejikuta wakiona elimu kama kimbilio pekee la kuepukana na mfumo dume. Itaendelea wiki ijayo,
0 Comments