LIVERPOOL ni miongoni mwa timu zinazotisha kwenye Ligi Kuu England msimu huu wa 2018/19. Kuna dalili timu hiyo inayofukuzana vikali na Manchester City kwenye nafasi za juu za ligi hiyo, inaweza kutimiza ndoto ya mashabiki wa timu hiyo ambao wana hamu ya ubingwa wa England ambao waliupata mara ya mwisho msimu wa 1989/90.
Msimu uliopita, Liverpool ilifanikiwa kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufungwa na Real Madrid 3-1 mjini Kiev, Ukraine.
Hata hivyo, Liverpool ilijizolea sifa kutokana na kucheza soka kali la kushambulia na kuifanya kutesa timu nyingine. Wakati msimu uliopita ilikuwa inasifika kutokana na kucheza soka kali la kushambulia sasa msimu huu imeamua kuweka nguvu katika kuimarisha safu yake ya ulinzi.
Mastaa wao Alisson Becker, Virgil van Dijk na Mohamed Salah wamefanya makubwa kutokana na kuifanya Liverpool inyanyase kwenye Ligi Kuu England. Liverpool imeongezea nguvu kikosi chake kwa kuwasajili wachezaji wapya Fabinho na Shaqiri msimu huu. Hata hivyo, pamoja na mafanikio ya timu hiyo, lakini hakuna mtu anayemtaja nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson.
Henderson aling’ara katika kipindi ambacho Liverpool inanolewa na Brendan Rogers kiasi ambacho gwiji wa zamani wa timu hiyo, Steven Gerrard alipoondoka basi alipewa unahodha wa timu hiyo.
Ni mchezaji mzuri wa kiungo, akisifika kwa pasi zake za uhakika, kuchezesha timu na pia ni mkali wa mashuti ya mbali. Kasoro anayolaumiwa nayo mara nyingi ni kupenda kwake kutoa pasi za nyuma na pia tabia yake ya kupenda kupiga mipira mirefu.
Tangu kutua kwa Jurgen Klopp, Henderson amekuwa akichezeshwa zaidi kama kiungo mkabaji ili kudhibiti mashambulizi ya timu pinzani. Anaheshimiwa ndani ya kikosi cha Liverpool, na pia ni mtu wa kutoa amri kwa wenzake na hana mzaha pale mchezaji anapokosea. Ila Henderson anasifika kutokana na uwezo wake wa kupokonya mipira na pia kutibua mashambulizi ya timu pinzani.
Mathalani katika mechi ya hivi karibuni kati ya Liverpool na Crystal iliyopigwa Januari 19, mwaka huu, Henderson ndio alikuwa mchezaji bora wa mechi ile kwa jinsi ambavyo alipigania ushindi wa timu yake. Kumbuka Liverpool ilipata ushindi wa mbinde kutokana na kuibuka na ushindi wa mabao 4-3.
Katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo, Liverpool ilicheza ovyo lakini Henderson ndiye aliyecheza kwa kujituma zaidi. Hata hivyo, staa aliyoeongelewa zaidi katika mechi ile alikuwa Salah, ambaye alipachika mabao mawili kwenye mchezo ule. Henderson alipiga soka ya kiwango cha juu kwenye mchezo ule, akitoa pasi 114 huku asilimia 94 zikifika kwa walengwa.
Mara nyingi alitibua mipango ya timu pinzani kwenye mchezo ule na kufanikiwa kwa asilimia 75 kupokonya mipira kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani. Henderson huwezi kumfananisha na wachezaji wa kiungo kama Pogba au Torreira lakini ana staili ya peke yake anapokuwa uwanjani.
Mathalani uhodari wake wa kupiga pasi ndefu pasi, ambazo mara nyingi hufikia wachezaji wenzake. Takwimu za Henderson msimu huu zinaonyesha amepiga jumla ya pasi 1,121 huku pasi ndefu zikiwa 69.
Henderson amepiga pasi za kupenyeza nne huku akiwa amepiga jumla ya krosi 14. Pia nahodha huyo wa Liverpool, ameokoa hatari za timu pinzani mara 109 huku akiwa ameondosha kwa kichwa mara nne.
Kiungo huyo wa Liverpool a m e t o l e w a mara moja kwa kuonyeshwa kadi nyekundu huku akiwa amefanya faulo mara 14. Hende-rson amepiga jumla ya mashuti saba msimu huu ingawa hakuna hata moja lililolenga goli.
MAKALA
0 Comments