Windows

Basi lapinduka, laua 4, lajeruhi 42

Picha

WATU wanne wamefariki na wengine 42 wamejeruhiwa baada ya basi la abiria la Kampuni ya Fikosh, walilokuwa wakisafiria, kupata ajali baada ya kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno alisema ajali hiyo ni ya juzi katika eneo la Mnarani wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma. Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, uliosababisha dereva wa gari hilo, Abdallah Ramadhani kushindwa kumudu gari katika mteremko wa eneo gari hilo lilipopindukia. Aliitaja gari hiyo ni aina ya scania lenye namba za usajili T AUV 400, iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Mwanza na Kigoma. Kwamba wakati ajali hiyo inatokea gari hiyo ilikuwa ikitokea Mwanza kupitia mkoa Tabora.

Kamanda Otieno alisema baada ya ajali hiyo, majeruhi walichukuliwa na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa Kigoma ya Maweni akiwemo dereva wa gari hilo, Abdallah Ramadhani. Walifikishwa Maweni baada ya kupatiwa huduma ya kwanza kwenye Kituo cha Afya Uvinza. Akizungumza kuhusu ajali hiyo jana mchana, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kigoma ya Maweni, Dk Osmund Dyegula alisema wagonjwa 22 ndiyo walikuwa wamebaki hospitalini, akiwemo mmoja ambaye hali yake ni mbaya. Mganga huyo alisema majina ya abiria waliofariki kwenye ajali hiyo, bado hawajatambua na kwamba maiti za abiria hao zimehifadhiwa chumba cha maiti cha hospitali hiyio ya mkoa.

Post a Comment

0 Comments