Windows

ARSENAL NA MAN UNITED VITA YA HESHIMA,MUDA UTAZUNGUMZA LEO


LEO Ijumaa, Arsenal itakuwa wenyeji wa Manchester United katika mchezo wa Kombe la FA utakaochezwa kwenye Uwanja wa Emirates.

Timu hizi zinapokutana kunakuwa na upinzani wa hali ya juu kuanzia nje ya uwanja kwa maana ya mashabiki mpaka ndani ya uwanja kwa wachezaji wenyewe.

Michuano hii tofauti na wanavyokutana kwenye ligi, hapa mtu akifungwa anaaga mashindano. Hali hiyo inazidisha mchezo huu kuwa na upinzani mkubwa.

Hakuna upande ambao utakuwa tayari kuona unapoteza mchezo kirahisi na kuaga mashindano ukizingatia kwamba zote zinatolea macho hapo ili tu msimu huu zisitoke mikono mitupu.

Kuanzia majira ya saa 4:45 usiku kwa saa Afrika Mashariki, mchezo huu ndiyo utaanza kuchezwa.



Rekodi zinaonyesha kuwa, mara ya mwisho kwa Arsenal kuifunga Man United ni Mei 7, 2017 katika mchezo wa Premier ambapo matokeo yalikuwa 2-0. Baada ya hapo timu hizo zimekutana mara tatu, Man United ikashinda mbili na sare moja.

Lakini katika Kombe la FA, mara ya mwisho kukutana kwa timu hizo ilikuwa ni Aprili 9, 2015 na Arsenal iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Rekodi za jumla zinaibeba Man United kutokana na kwamba timu hizo zimekutana mara 228. Man United imeshinda 98, sare 48 na imefungwa 82.

Katika Kombe la FA pekee, kabla ya leo timu hizo zimekutana mara 15, Man United imeshinda saba, Arsenal nayo imeshinda saba na sare moja.

Mashabiki wa Man United wanaamini kwamba kikosi chao kina nafasi kubwa ya kushinda leo kutokana na wimbi la ushindi walilonalo tangu kuondoka kwa Jose Mourinho na nafasi yake kuchukuliwa na Ole Gunnar Solskjaer.

Vijana wa Arsenal wanaonolewa na Unai Emery, wanataka kushinda mchezo huu ili kujitengenezea nafasi ya kulitwaa kombe hilo ambalo msimu uliopita ililikosa baada ya kulitwaa kwa misimu mitatu mfululizo.

Kinachosubiriwa ni kwamba, wimbi hilo la Man United kushinda mechi zake tangu kuondoka kwa Mourinho litaendelea au la, lakini pia Arsenal nayo itaendelea kushinda kama ilivyokuwa mara ya mwisho zilipokutana kwenye michuano hii? Tusubiri muda utazungumza.

Post a Comment

0 Comments