Windows

Kotei afunguka sababu za kuitosa Yanga




Kwanza amekiri Yanga kutaka huduma yake pamoja na mazungumzo baina ya pande hizo mbili, lakini akaweka wazi kuwa heshima aliyopewa na mashabiki na viongozi wa Simba ni ngumu kuivunja.

WAKATI mabosi wa Yanga wakimalizana na wenzao wa Kaizer Chiefs ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ili kuinasa huduma ya kiungo wao mkabaji James Kotei, mambo bado yanaonekana kuwa magumu.
Yanga kupitia kwa wadhamini wao kampuni ya GSM, walimtuma mkurugenzi Hersi Said kuzungumza na Chiefs ambao walikubali kumuachia Kotei kutua Yanga, lakini tatizo likabaki kwa kiungo huyo wa Ghana kukubaliana na dili hilo.

Mwanaspoti ambalo limekuwa likifuatilia hatua kwa hatua mchakato wa Yanga kumnasa kiungo huyo limebaini kwamba, waajiri wa zamani wa kiungo huyo, Simba wameingilia kati na kutibua mpango mzima.

Kotei, ambaye aliachana na Simba mwishoni mwa msimu uliopita amekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya mabosi wa Simba na mashabiki ambao hawatamani kuona dili hilo likitiki kama ilivyokuwa kwa Haruna Niyonzima aliyerejea Yanga kwenye dirisha dogo la usajili.

Hata hivyo, Mwanaspoti limezungumza moja na kwa moja na Kotei kutoka Afrika Kusini ambapo amefunguka kila kitu kuhusu mchakato wa kurejea Ligi Kuu Bara akiwa ndani ya jezi ya Yanga.
Kwanza amekiri Yanga kutaka huduma yake pamoja na mazungumzo baina ya pande hizo mbili, lakini akaweka wazi kuwa heshima aliyopewa na mashabiki na viongozi wa Simba ni ngumu kuivunja.

Amesema wakati akiwa nchini kuichezea Simba alikuwa mmoja wa wachezaji wanaopendwa na mashabiki wa klabu hiyo na kwamba, anajisikia vibaya kurejea nchini kukipiga na klabu nyingine tofauti na Wekundu wa Msimbazi.

“Ni kweli Yanga wananitaka sana na kuna mazungumzo wamefanya na Chiefs, lakini nikiwa huko Tanzania nimetengeneza heshima kubwa sana kwa viongozi na mashabiki wa Simba,” akasema.
“Walionyesha upendo wa dhati kwangu na hata baada ya kuondoka bado tunawasiliana mara kwa mara na wanatamani siku moja nirudi.”

“Ukweli ni kuwa nilimuita wakala wangu wakati wa majadiliano na naweza kusema sivutiwi na mpango wa kwenda Yanga kwa sababu ya heshima ya Simba…kama ni klabu nyingine nitakuwa tayari iwe kwa mkopo ama kuuzwa,” alisema Kotei, ambaye pia amefichua kuwa kabla ya kumaliza mkataba wake aliwapa nafasi mabosi wa Simba kuweka bayana kama watamuongezea ama watamruhusu kuondoka.

Pia, amesema kuwa ana ofa tatu mezani za pesa nono ikiwemo ya Yanga, ambao wamekuwa wakipambana kuona dili hilo linakamilika ila kikwazo ni upendo na thamani aliyopewa na mashabiki na viongozi wa Simba.

PESA SI KILA KITU
Katika kuonyesha kuwa mahaba yake kwa Simba yamezidi kipimo, Kotei amefunguka kuwa wamemuwekea ofa nono mezani ya pesa nyingi ambayo inaweza kumsaidia katika maendeleo, lakini wakati mwingine pesa siyo kila kitu katika maisha.

“Sikiliza nikwambie rafiki yangu, ukweli Yanga wanataka kunilipa pesa nzuri sana, lakini ukweli ni kuwa pesa siyo kila kitu katika maisha kwani wakati utu ni bora kuliko jambo lolote.
“Sikuwa nawaza pesa zaidi na kwangu pesa siyo kila kitu hata kama Yanga wangeongeza mara mbili ama tatu, ndio sababu nimefanya maamuzi haya,” alisema Kotei.

WASIKIE VIONGOZI
Wakati mchakato wa Kotei kutua Yanga ukionekana kutibuka, Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kuwa mkakati wa kiongozi mmoja wa Simba kuombwa na watani zao wa jadi kumshawishi Kotei akubali nao umekwama.

“Jamaa (bosi mmoja wa Yanga) aliniambia nijaribu kuzungumza na Kotei akubali kutua Jangwani kwa sababu Kaizer (Chiefs) na wakala wake hawana shida ila mwenyewe ameweka ngumu kabisa.
“Nilijaribu kuongea na Kotei kumuuliza tu ukweli wa jambo hili, lakini inaonekana ameshafanya uamuzi wa kugomea ofa licha ya kuwa na pesa nyingi,” alisema bosi mmoja wa Simba ambaye aliomba jina lake lisiwekwe wazi.


Post a Comment

0 Comments