Kwa ushindi huo, Simba itaivaa Mtibwa Sugar katika fainali itakayopigwa keshokutwa Jumatatu kwenye uwanja huo huoA
SIMBA imetinga katika fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa kuwafunga mabingwa waliokuwa mabingwa watetezi, Azam FC kwa penalti 3-2 baada ya dakika tisini za mchezo kumalizika kwa sare ya bila mabao kwenye Uwanja wa Amaan.
Kwa ushindi huo, Simba itaivaa Mtibwa Sugar katika fainali itakayopigwa keshokutwa Jumatatu kwenye uwanja huo huo.
Lakini mjadala mkubwa ulikuwa ni kipa wa Azam, Razak Abalora, ambaye alidaka penalti mbili ya Sharaf Eldin Shiboub na ya Meddie Kagere, lakini akakosa penalti ya tano ya timu yake na kushuhudia wakisukumwa nje ya michuano hiyo.
Mchezo ulivyokuwa
Simba ndio waliotawala karibu vipindi vyote wakicheza soka lao la pasi nyingi na dakika ya saba tu Hassan Dilunga alipoteza nafasi nzuri akiwa ndani ya eneo la hatari shuti lake linatoka nje kidogo akipokea pasi safi ya Meddie Kagere.
Dakika ya 9 Simba walifanya shambulizi jingine zuri kwenye lango la Azam, lakini Ibrahim Ajibu shuti lake zuri lilipanguliwa na kipa wa Azam, Abalora kisha mpira kurudi tena kwa mpigaji lakini shuti lake likapaa juu ya lango.
Dakika 11 Abalora aliibeba tena Azam kwa kupangua krosi safi ya Francis Kahata iliyokuwa inasubiriwa na Kagere aweke wavuni.
Muda wote Azam walionekana kukosa maarifa ya kutengeneza mashambulizi wakizidiwa vikali katika eneo la kiungo.
Dakika ya 24 Azam walilifika lango la Simba kwa mara ya kwanza lakini shambulizi lao kupitia krosi ya nahodha wao Bruce Kangwa lilidhibitiwa vyema na mabeki wa Simba.
Azam dakika ya 32 walipiga shuti la kwanza lililolenga lango pale beki Nicholas Wadada alipofumua shuti kali lililopanguliwa na kipa Benno Kakolanya na mpira kumtoka na kuwa kona iliyokosa madhara.
Kiungo Brayson Raphael wa Azam alifanya kazi nzuri kuucheza mpira wa pasi ya Kagere aliyekimbia vyema na mpira akipokea pasi safi ya Sharaf Shiboub na kama pasi ya Kagere ingemfikia Ajibu alikuwa anafunga kirahisi.
Dk ya 45 Simba ilipoteza nafasi nzuri mpira wa adhabu ndogo wa ajibu ulitoka nje kidogo ya eneo la hatari uligonga ukuta na kutoka nje inakuwa kona iliyokosa madhara, adhabu hiyo ilitokana na wadada kumuangusha Hassan Dilunga dakika ya 44.
Mpaka mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili Simba walirudi na kasi yao ileile dakika ya 47 beki Mohamed Yakubu alifanya kazi nzuri kuidhibiti pasi ya Kagere ikimtafuta Kahata.
Dakika ya 50 Simba waliendelea kuliandama lango la Azam wakipigiana pasi safi Kagere, Dilunga na Shiboub lakini shuti la Kagere lilidakwa vyema na Abalora.
Beki wa Simba, Pascal Wawa almanusura aiumize timu yake pasi yake mbovu ilinaswa na Obrey Chirwa lakini shuti lake linakatika hewani na kutoka nje kidogo.
Azam dakika ya 67 walifanya shambulizi zuri kuliko yote tangu mchezo uanze Chirwa alishindwa kuunganisha wavuni kidogo krosi ya kiungo Joseph Mahundi aliyefanya kazi ya kuwatoka mabeki wa Simba.
Mpaka mwisho wa mchezo hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na kuufanya mchezo huo kuamuriwa kwa mikwaju ya penalti.
Penalti zilivyokuwa
Katika hatua ya penalti ndipo mshindi alipopatikana kwa Simba kuibuka washindi kwa jumla ya penalti 3-2.
Simba waliingia fainali kwa shukrani ya penalti za beki Erasto Nyoni, John Bocco, Jonas Mkude waliofanikiwa kupata huku Shiboub na Kagere penalti zao zikichezwa na Abalora.
Abalora ambaye alionekana angekuwa shujaa wa mchezo alijiharibia mwenyewe baada ya kukosa penalti ya mwisho aliyopiga lakini ikapanguliwa na Kakolanya. Idd Kipagwile aligongesha nguzo la lango na Donald Ngoma alipaisha penalti.
Kwa matokeo hayo sasa Simba inaifuata Mtibwa Sugar katika mchezo wa fainali utakaopigwa Jumatatu
Vikosi:
Simba: Beno Kakolanya, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Sharaf Shiboub, Hassan Dilunga/Rashid Juma (dk.80), Francis Kahata/Luis Maquissone (dk.70) Ibrahim Ajib, John Bocco (dk.70) na Medie Kagere
Azam: Razack Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakub Mohammed, Abdallah Heri 'Ssebo' Oscar Masai (dk. 64), Bryson Raphael, Joseph Mahundi, Masoud Abdallah 'Cabaye', Shaaban Chilunda/ Kassim Hamis (dk.72), Obrey Chirwa/Donald Ngoma (82) na Iddi Selemani 'Nado'/ Idd Kipagwile (dk.76).
0 Comments