Kwa mara ya kwanza jana mashabiki wa Yanga walimshuhudia mlinzi kiraka Ally Mtoni 'Sonso' akicheza nafasi ya kiungo mkabaji kwenye mchezo dhidi ya Alliance Fc
Katika mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, Mtoni alicheza kiungo cha ulinzi huku nahodha Papy Tshishimbi akisogezwa mbele kuchezesha timu
Mwanzoni mashabiki walionyesha mashaka baada ya kikosi kuwekwa hadharani, lakini labda wengi hawakufahamu kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Mtoni kucheza nafasi hiyo
Katika klabu yake ya zamani Lipuli Fc Mtoni alicheza nafasi zote za ulinzi pamoja na hiyo ya kiungo
Hata yeye mwenye mara kadhaa amebainisha kuwa anamudu kucheza nafasi zote za beki pamoja na kiungo bila ya wasiwasi wowote
Jana Mtoni alionyesha utulivu pamoja na umahiri wa kupiga pasi za uhakika
Ni nafasi ambayo kama ataendelea kuaminiwa anaweza kufanya vizuri zaidi pengine kuliko hata anapocheza beki wa kushoto
Katika nafasi hiyo hakuwa mzuri katika kushambulia lakini aliipa timu uwiano mzuri kwenye kujilinda
Pengine ni moja ya jitihada ambazo kocha Charles Mkwasa anachukua ili kuimarisha safu yake ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao saba baada ya kushuka dimbani mara saba
Kwani majukumu makuu ya kiungo mkabaji ni kulinda safu ya ulinzi, kuchezesha timu na kwenda kushambulia kama italazimu
Mkwasa anapendelea kuwa na kiungo mmoja ambaye anabaki kuwasaidia mabeki mfumo ambao ni tofauti na mtangulizi wake Mwinyi Zahera ambaye alipendelea zaidi kucheza 'toto football' ambapo viungo wote walilinda na kwenda kushambulia
0 Comments