Windows

Zahera ajilaumu mwenyewe

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera, amesema kuwa lawama zote anazibeba yeye huku akiitaja sababu ya kipigo cha mabao 2-1 walichokipata walipocheza na Zesco United ya Zambia.

Kipigo hicho kimewaondoa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2 na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Yanga ilicheza na Zesco katika mchezo wa Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo mikubwa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema kitendo cha yeye kuchelewesha kufanya mabadiliko ndiyo sababu wa kupoteza mchezo huo.

Zahera alisema kuwa alichelewa kufanya mabadiliko kutokana na baadhi ya wachezaji kuwepo kwenye mipango yake ya kupiga penalti kama ungemalizika kwa sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.

 

Alimtaja kiungo wake Abdulaziz Makame aliyejifunga bao la pili ndiye alitakiwa kuwa mchezaji wa kwanza kumfanyia mabadiliko, lakini kutokana na mipango yake ya kutaka kumtumia kwenye penalti akambakisha kabla ya kujifunga bao hilo.

“Makame hatakiwi kupewa lawama yoyote baada ya kujifunga, lawama hizo nazibeba mimi niliyembakisha kucheza kwa dakika 90 akiwa amechoka.

 

“Lakini sikutaka kumtoa kutokana na umuhimu wake kwenye upigaji wa penalti, ni mpigaji mzuri wa penalti na nilitarajia mchezo huo ungeenda katika penalti.

“Kama ningewahi kufanya mabadiliko mapema ya wachezaji wangu waliokuwa wamechoka wa safu ya kiungo Fei Toto (Feisal Salum) na Makame, niamini matokeo yasingemalizika ya kufungwa mabao 2-1.

 

“Niwapongeze wachezaji wangu waliocheza kwa kujituma na kufuata maelekezo yangu na kufanikiwa kumiliki mpira katika dakika zote 90, tunarejea kwenye Shirikisho hivi sasa akili zote nazielekeza huko na kikubwa ninataka kuona tukifanya vizuri,” alisema Zahera.

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

The post Zahera ajilaumu mwenyewe appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments