Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati), akimsikiliza Katibu wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaj na Bodaboda Mkoa wa Kilimanjaro (CWBK), Rashid Omary, alipokuwa anatoa pongezi kwa Waziri huyo, kuwasaidia kupata eneo la maegesho ya Bajaj na Bodaboda Shairifu, Mjini Moshi, leo. Mwezi uliopita, Lugola alitatua mgogoro uliopo kati ya Manispaa ya Moshi na CWBK kuhusiana na maeneo ya maegesho. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Khamis Issa, na wapili kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani humo, Zauda Mohammed. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (aliyevaa Kaunda suti), akikagua eneo la maegesho ya Bodaboda na Bajaj, Sharifu, Mjini Moshi, leo. Lugola aliambatana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Khamis Issa (kulia), kukagua maeneo ya Aghakan na Shairifu ambalo lilileta mgogoro kati ya Manispaa ya Moshi na Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaj na Bajaj Mkoani humo (CWBK), na kutatuliwa na Waziri huyo mwezi uliopita, mjini humo. Wapili kushoto ni Katibu wa CWBK, Rashid Omary. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimuaga Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaj na Bodaboda Mkoa wa Kilimanjaro (CWBK), Rashid Omary, mara baada ya kumaliza kukagua vituo vya Sharif una Aghakan vya maegesho ya Bodaboda na Bajaj, Mjini Moshi, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akimuaga Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohammed (kushoto), mara baada ya Waziri huyo, kumaliza kukagua vituo vya Sharif una Aghakan vya maegesho ya Bodaboda na Bajaj, Mjini Moshi, leo. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa huo, Khamis Issa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………..
Na Felix Mwagara, Moshi (MOHA).
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelitaka Jeshi la Polisi Kikosi Usalama Barabarani washirikiane na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuzisajili bodaboda na bajaj zote nchini ili ziweze kudhibitiwa katika ukusanyaji wa faini pamoja na matukio mbalimbali ya kiuhalifu zinapofanya makosa.
Lugola alisema ushirikiano kati ya viongozi au askari waliopo chini ya halmashauri nchini ipo ndani ya sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura namba 322, hivyo Jeshi lake linapaswa kushirikiana na Polisi Wasaidizi waliopo chini ya halmashauri ya Miji, Wilaya, Manispaa na Jiji kwa mujibu wa sheria.
Waziri Lugola ameyasema hayo Mjini Moshi, leo, wakati alipokuwa anakagua vituo vya bodaboda na bajaj mjini humo ambapo mwezi uliopita alifanya mkutano na wamiliki na waendesha bodaboda na bajaj mkoani humo kwa lengo la kutatua migogoro mbalimbali waliokuwa wanailalamikia Manispaa ya Moshi kuwanyanyasa pamoja na kuwafukuza kuegesha kituo cha Sharif una Aghakan mjini humo ambapo Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabara Mkoani humo aliwaelekeza wawepo katika eneo hilo.
“Askari wa usalama barabarani, muache visingizio kuwa ukamataji wa bodaboda ni mgumu hasa mnapowaandikia makosa walipe baada ya siku saba, mara usingizia bodaboda hazipo katika mfumo wa TRA kama magari, tukiziachia tuzipate wapi, nilishawaelekeza mshirikiane na viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijijini, Miji, Manispaa na Jiji kuanzisha kanzi data, kwenye mfumo wa kuwasajili waendesha bodaboda wote sehemu mbalimbali nchini, na taarifa za bodaboda hizo endapo zinafanya makosa inakua rahisi kuzikamata kwasababu zipo kwenye mfumo,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, lengo la usajili wa bodaboda huo, ni kutokana na kuepuka kuzikamata hovyo na kuziweka vituoni jambo ambalo analipinga kuepusha mlundikano wa boaboda vituoni na pia kuwasababishia bodaboda hao kuwaongezea umaskini zaidi.
“Naomba niendelee kurudia tena agizo hili, bodaboda zinazopaswa kuwepo vituo vya polisi ni za aina tatu, moja bodaboda zilizotumika katika matukio ya uhalifu, mbili zilizohusika katika ajali, na tatu bodaboda zilizookotwa, mbali na makundi hayo zinapaswa kulipwa faini,” alisema Lugola.
Pia Lugola aliwataka baadhi askari na wananchi kuacha tabia ya kuwatuhumu viongozi wanapowatetea waendesha bodaboda wanaambiwa kuwa wanasiasa ndiyo wanasababisha ajali kuongezeka.
Amesema kauli hiyo sio sahihi, kwani wanaosababisha ajali asilimia 76 kwa mujibu wa utafiti wa ajali zinazotokea barabarani zinasababishwa na makosa ya wanadamu na sio bajaj na bodaboda peke yao, na asilimia 24 za ajali zinatokea zinasababishwa na ubovu wa miundombinu.
“Kumekuwa na dhana potofu kwamba wanasiasa kama mimi tunasababisha ajali za bodaboda, kwasababu tunawatumia bodaboda kwa mgongo wa siasa, sasa nataka niwaambie, wanaosababisha ajali barabarani ni asilimia 76 ni makosa ya wanadamu ambao ni wanadamu watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, wenye mikokoteni, wanafuga mifugo barabarani na madereva ndio wanasababisha ajali, na sio bodaboda wala bajaj peke yao,” alisema Lugola.
Lugola amesema hakuna mahali popote ambayo tumesema baodaboda wakifanya makosa wasikamatwe, tunachosema na kusimamia nikupunguza umaskini kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo inaelekeza Bodaboda na Bajaj wafanye biashara ili wapunguze umaskini.
Aidha, Lugola amesema Serikali ya Magufuli inataka wananchi Watanzania wajiajiri hivyo sekta ya bodaboda lazima iheshimika kwakua nao wanatafuta ridhiki kama ilivyo kwa watanzania wengine.
0 Comments