Paris, Ufaransa. HAINA siri. Wanasoka ni baadhi ya watu wanaolipwa pesa nyingi sana duniani. Kutokana na hilo, wamekuwa wakiishi maisha wanayopenda wao. Starehe na kumiliki wanachokitaka.
Kuna baadhi ya wanasoka hao wamekuwa wakilipwa pesa nyingi sana, kama vile supastaa wa Kibrazili, Neymar na huduma yake anayotoa huko Paris Saint-Germain.
Neymar anamiliki anachokitaka. Kuhusu usafiri ndio usisema, magari ya kifahari kama yote. Neymar amefika mbali zaidi kwenye usafiri, anamiliki boti binafsi na kali zaidi, hadi ndege anayo.
Hivyo ni suala la dakika chache tu, Neymar akaamua kutoka zake Paris kwenda kutua huko Rio de Janeiro kula bata. Ndege yake ipo tayari muda wote.
Dili la kutoka Barcelona kwenda PSG lilikuwa la pesa ndefu kwa staa huyo, ambaye kwa sasa anahusishwa na mpango wa kurudi huko Nou Camp.
Kama ambavyo ililipwa Pauni 198 milioni kunasa saini yake, hata mshahara Neymar aliokwenda kulipwa huko Paris si wa mchezomchezo. Si chini ya Pauni 700,000 kwa wiki.
Jambo hilo lilimfanya Neymar kuona wazo la kununua ndege binafsi ni dogo tu kwake, akanunua kujirahisishia usafiri.
Ndege anayomiliki Neymar inaitwa Cessna Citation Sovereign Plus. Manunuzi ya ndege hiyo yalimwingiza Neymar kwenye matatizo na watu wa kodi ya mapato.
Sakata hilo, baadaye lilimfanya akutwe na hatia ya kudanganya kuhusu bei aliyonunulia kama kiasi cha Dola 52 milioni.
Kutokana na hilo, serikali waliamua kuishikilia boti yake binafsi na ndege yake ya mwanzo kabisa, Embraer 100.
Kwenye jambo hilo, Neymar ilibidi afanye mambo mengi kumaliza tatizo ikiwamo , aliamua kuweka mambo sawa na kampuni yake ya Neymar Sport E Marketing, kuimiliki ndege hiyo.
Ndege hiyo ya Neymar ina uwezo wa kuchukua abiria 12. Ndani kuna mambo mengi, ambayo hakika ukipanda hutokuwa na haraka ya kutaka kushuka.
Lakini, kwenye ndege hiyo, unaweza kufanya sherehe ya watu 19 na mambo yakaenda sawa tu.
Hata ukitaka kumtoa mpenzi wako, basi ndani ya ndege hiyo kuna vyumba maalumu, ambavyo vitakudanya ule msosi wowote ule iwe kifungua kinywa, mlo wa mchana au usiku bila wasiwasi na katika mazingira yenye mvuto.
Kuna sehemu inayoweza kutazama mechi ya mpira hata kama ukiwa angani, hivyo Neymar wala hana shida anaweza kuwa safarini na kuendelea kutazama mechi ya soka akiwa angani.
Ukisikia watu wanakula bata la maana, basi ndio hilo, unakuwa angani, lakini unapata kila kitu kinachoendelea ardhini. Kuna sehemu ya kupashia misosi moto na kuweka vinywaji baridi. Ukiwa ndani ya ndege ya Neymar, utajua maana halisi ya kuishi kwa kustarehe!
0 Comments