Muite Meddie Kagere baada ya kuanza ligi kwa kufunga mabao mawili amesisitiza kuwa sasa anataka kufunga kila mchezo atakaocheza ukiwemo ule wa watani zao, Yanga.
Kagere ambaye ni raia wa Rwanda, msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu akitupia mabao 23 kimiani na juzi ameanza kuhesabu akaunti yake ya mabao baada ya kufunga mawili dhidi ya JKT Tanzania katika ushindi wa mabao 3-1 ambao Simba ilipata.
Kagere alisema kuwa kikubwa alichopanga ni kutumia vema kila nafasi atakayoipata ya kufunga mabao katika mechi ya ligi ili kuhakikisha anatimiza malengo aliyojiwekea ya kuutetea ubingwa wa ligi, pia kulichukua Kombe la FA.
Aliongeza kuwa tofauti na majukumu aliyonayo ya kufunga mabao, pia amepanga kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wenzake bila ya kuangalia ufungaji bora anaoutetea katika msimu huu.
“Nafahamu mashabiki wa Simba bado wanamaumivu ya kuondolewa Caf ambayo sisi yanatuumiza na yatachukua muda mrefu kuondoka kichwani mwetu, kwani tulikuwa tuna matarajio makubwa ya kufika mbali Caf zaidi ya msimu uliopita.
“Lakini ndiyo matokeo, hivyo basi hasira zangu zote nazielekeza kwenye ligi na kama mshambuliaji nachukua majukumu yote ya kuhakikisha timu inapata ushindi ili tuutetee ubingwa wa ligi, pia kuchukua Kombe la FA.
“Hivyo, nilichopanga ni kutumia vema kila nafasi nitakayoipata uwanjani ikiwemo kufunga na kutengeneza mabao bila ya kuangalia ufungaji bora kwangu siyo muhimu sana.
“Muhimu kwangu ni kuchukua makombe ambacho ndiyo kitu cha msingi kilichonileta Simba, hayo mengine yatajulikana mwishoni mwa msimu ikitokea nimekuwa mfungaji bora, basi nitashukuru,” alisema Kagere.
0 Comments