KUELEKEA mchezo wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United, mabosi wa Yanga haraka wamepanga kumleta mtaalam wa saikolojia ili kuhakikisha wanapata ushindi wa pili ugenini.
Yanga imepanga kwenda kuweka kambi Septemba 23, mwaka huu kabla ya mchezo huo utakaopigwa Septemba 28 kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa kwenye Mji wa Ndola nchini Zambia.
Katika mchezo huo Yanga watalazimika kupata ushindi wa aina yoyote au sare ya zaidi ya bao 1-1 ili wafuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa Afrika ngazi ya klabu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa na kuthibitishwa na katibu wa kamati ya hamasa ya timu hiyo, Deo Mutta, maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri huku wakipanga kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanafakiwa kupata ushindi ugenini.
Mutta alisema kuwa wikiendi hii kabla ya timu kuanza safari ya kuelekea Zambia, wamepanga kukutana na wachezaji wao kwenye moja ya hoteli nchini kwa ajili ya kufanya kikao sambamba na kupewa somo na mmoja wa wataalam wakubwa wa saikolojia.
Aliongeza kuwa lengo ni kuwatengeneza kisaikolojia ili wachezaji hao wajenge hali ya kujiamini watakapokuwepo uwanjani wakivaana na Zesco katika mchezo huo wa marudiano.
“Tumejifunza mengi katika michuano hii mikubwa ya kimataifa na hasa katika michezo ya hapa nyumbani ambayo imekuwa migumu kwetu kupata matokeo mazuri ya ushindi.
Hiyo inatokana na mashabiki wetu kutaka matokeo mazuri kwa haraka hali inayosababisha wacheze kwa hofu na presha kubwa, hiyo ndiyo sababu kubwa sisi tusifanye vizuri nyumbani na kingine mechi zetu kuchezwa na baadhi wapinzani wetu ni lazima ugumu utakuwepo.
“Tunakwenda Zambia ni matarajio yetu kuona timu inarejea nyumbani kwa ushindi na hilo linawezekana kabisa, tayari tumeanza maandalizi hayo kwa kuanzia na wachezaji ambao wikiendi hii tunatarajia kukutana nao kama viongozi pamoja na mtaalam wa saikolojia.
“Kazi kubwa ya mtaalam huyo ni kuwajengea hali ya kujiamini kwamba inawezekana timu kupata matokeo mazuri ya ushindi, licha ya hapa nyumbani kupata sare ya bao 1-1 na hilo liwezekana kwao kama waliweza kuwafunga nyumbani Township Rollers ya Botswana,” alisema Mutta.
The post Mtaalam Mpya Ashushwa Yanga appeared first on Global Publishers.
0 Comments