MSEMAJI wa Klabu ya Simba, Haji Manara ameomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali madai ya Sh milioni 83 dhidi yake, akidai kwamba anaidai kampuni hiyo ya Oman inayotengeneza manukato ya Dela Boss Sh milioni 31.
Majibu hayo ya Manara yametokana na kesi iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Kampuni ya Abu Masoud Al Jahdhamy LLC dhidi yake na wenzake.
Katika majibu yake ya utetezi Manara anadai Kampuni hiyo anaidai Sh milioni 31 ikiwa ni asilimia 30 ya faida kutoka na matangazo ya manukato hayo ya Dela Boss.
Manara na wenzake wanapinga madai ya mdai ya kwamba waliingia mkataba wa ubia na kumtaka athibitishe hilo.
Anadai Manara alikuwa balozi na mwanahisa , alitangaza bidhaa hiyo katika mitandao ya kijamii, Twitter, Facebook, Instagram, YouTube, Snapchat and WhatsApp.
Manara anadai walikubaliana na mdai watagawana faida ya mauzo ya manukato hayo.
Mlalamikaji katika kesi hiyo ni Abu Masoud Al Jahdhamy LLC amefungua shauri hilo akiomba walalamikiwa, Manara, Beatrice Ndungu na Palm General Supply waamuliwe kumlipa Sh milioni 83 na fidia nyingine itakayoona inafaa na gharama za mawakili.
Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Wanjah Hamza. Katika madai ya msingi, mlalakaji anadai walalamikiwa fedha hizo baada ya kuwasambazia bidhaa yenye nembo ya Dela Boss Perfume ‘Tanzania’ zilizotengenezwa Dubai.
Ilidaiwa kuwa mlalamikaji aliingia mkataba na Manara Desemba 19,2018 kwa kuchapa bidhaa zenye maneno hayo.
Katika mkataba huo, mlalamikaji alitakiwa kupata 70% na Manara 30% na kwamba faida itakayopatikana angemrudishia mlalamikaji hiyo gharama za uwekezaji wa kufikisha bidhaa jijini Dar es Salaam.
Januari 21,2019 mlalamikaji kupitia kampuni ya AMA Trading LLC ilituma hizo bidhaa jijini Dar es Salaam ambazo zina thamani ya Sh Milioni 46 na zilipokelewa na mlalamikiwa wa pili, Ndungu na wa tatu kama mawakala.
Januari 21,2019 mlalamikaji alituma hati ya malipo ya Sh 83,300,000 kwa mlalamikiwa wa pili na wa tatu akitaka kulipwa faida ya uwekezaji na kiasi kilichotumika kununulia bidhaa hizo pamoja na faida.
Walalamikiwa walipokea bidhaa hizo na kwamba mpaka sasa hawajalipa chochote pamoja na kudaiwa kwa maneno na maandishi kutoka kwa mlalamikaji.
Mlalamikaji anadai kuwa kutokana na kitendo hicho kimemsababishia usumbufu mkubwa na hasara katika biashara zake.
0 Comments