Windows

Viongozi wa SADC Tanzania ni Nyumbani kwao - Dkt Abbasi


Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Hassan Abbasi amesema kuwa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika- SADC kwa viongozi Tanzania ni nyumbani.

Akizungumza katika Kipindi cha 360 cha Clouds TV, Dkt. Abbasi amesema kuwa Tanzania ina historia kubwa kwa nchi za kusini mwa Afrika tokea enzi za ukombozi wa nchi hizo, ambapo Tanzania ilitumika kama kitovu cha wapigania uhuru.

“Viongozi hawa wengi wanarudi nyumbani, ikumbukwe kuwa Tanzania ndiyo ilikuwa moja kati ya mataifa matatu yaliyoasisi kamati ya Ukombozi ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Tanzania ndiyo ilikuwa Makao Makuu ya ukombozi na Ofisi Kuu ya ukombozi ipo Jijini Dar es Salaam, kwa hiyo hii ni hitoria kubwa kwa nchi yetu”, Dkt.Abbasi.


Dkt.Abbasi amesema kuwa Mkutano huu ambao ni fursa kwa watanzania maandalizi yake yamekamilika na sasa Tanzania ipo tayari kuwakaribisha wageni kutoka nchi wanachama wa SADC, huku baadhi ya mambo yakikamilishwa na kamati ya maandalizi kutoka SADC, Serikali ya Tanzania, wabia wa SADC pamoja na Sekta binafsi.

Aidha, Dkt. Abbasi amesema kuwa nchi za SADC zimekuwa na ajenda kubwa ya kutekeleza ujenzi na kuimarisha viwanda Jambo ambalo alisisitiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli wakati wa ufunguzi wa maonesho ya nne ya wiki ya viwanda ya Nchi wanachama wa SADC.

“Mhe.Rais Magufuli anaamini kwenye Sera ya Viwanda kama Tanzania tunavyotekeleza Sera hii, siyo kwa Tanzania tu bali hata kwenye nchi wananchama wa SADC. Rais ata sukuma maendeleo ya viwanda kwani atakuwa Mwenyekiti wa SADC, na kama mnavyojua nchi wanachama wanatengeneza ajenda kuhusu ukuaji na uimarishaji wa viwanda”, Dkt.Abbasi.

Amesema kuwa viwanda ndiyo nguzo ya Maendeleo kwa nchi wanachama na kama Rais Magufuli, alivyosisitiza kuwa Afrika lazima ifanye biashara yenyewe kwa yenyewe badala ya kutegemea kufanya biashara na Nchi za Ulaya. Hivyo, SADC ni fursa kwa nchi wanachama kununua na kuuza bidhaa kwenye jumuia, kama nchi inahitaji mahindi basi Tanzania iuze mahindi yake ndani ya Jumuiya ili kukuza soko.

Dkt.Abbasi alisema kuwa Rais Magufuli amekuwa ni kiongozi ambaye anasimamia yale anayoyaamini ili kuwaletea Maendeleo wananchi wake kwa hiyo sasa atakwenda kusukuma utekelezaji wa ujenzi wa viwanda kwa nchi wanachama.

“Kuna mwanahistoria mmoja anaitwa Walter Rodney ambaye aliandika kitabu kushusu namna gani mataifa ya Ulaya yanayadidimiza mataifa ya Afrika, lakini pia unaona siku ile Rais anaongea na kukubaliana na msomi mwingine aliyeandika kuwa namna gani Afrika inajididimiza kwa hiyo msimamo wake utaifanya Tanzania na SADC kutekeleza ujenzi wa viwanda akiwa kama mwenyeketi wa Jumuiya hiyo kwa mwaka mmoja”, Dkt.Abbasi.

Dkt.Abbasi alisema kuwa nchi za SADC zinatakiwa kuwa na viwanda vya kuchaka malighafi na kuzalisha bidhaa ili kuongeza thamani, akitolea mfano wa mahindi ukiuza bila kuchakatwa hindi moja shilingi 200. Lakini kumbe likiwa limechatwa na kuzalisha unga unaweza ukauza kilo moja kwa shilingi 2,000, kwa hiyo ajenda ya kujenga viwanda vya kuchakata mazao itasimamiwa vema itakuza thamani ya bidhaa ndani na Nje ya Jumuiya.

Dkt. Abbasi alisema kuwa watanzania wengi sasa wameamka na Serikali ambacho inafanya ni kuwawezesha waamke na kuchangamkia fursa za biashara ndani ya SADC. Alitolea mfano kwenye maonesho ya SADC ambayo yanaendelea Jijini Dar es Salaam kuwa wapo watanzania ambao wanaonesha bidhaa zao wanazopeleka SADC.

“Takwimu zinaonesha watanzania tumeaka sana kwenye soko la SADC, tumepeleka bidhaa zinazofikia dola za kimarekani milioni 900 na tumengiza bidhaa zinazokadiriwa kufikia Dola milioni 600, kwa hiyo sisi bado kitakwimu tumechangamka zaidi kwenye soko la SADC.

Dkt.Abbasi alisema kuwa Serikali imeweka mikakati kwa Taasisi zinazohusisha masula ya biashara ikiwemo Tantrade na Bodi ya Masoko ya Mazao Mchanganyiko, kuitafuta masoko na kufanya utafiti ili kuwasaidia wafanyabiashara.

Post a Comment

0 Comments