Windows

KIKOSI YANGA CHAFUMULIWA, ZAHERA AHUSIKA


KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera ameamua kufumua kikosi chote huku akisisitiza kwamba hafanyi mambo kufurahisha mashabiki. Zahera amekwenda mbali na kusisitiza kwamba hata katika mechi ya kirafiki leo(jana) Jumapili dhidi ya AFC Leopards hakuna hata mchezaji mmoja aliyecheza Moshi dhidi ya Polisi Tanzania atakayeanza.

Katika mechi dhidi ya Polisi juzi Ijumaa Yanga ilifungwa mabao 2-0 huku ikianzisha sura nyingi mpya.

Zahera amekwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba hata kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Township Rollers hakuna mchezaji yoyote aliyecheza dhidi ya Polisi ataanza.

Kikosi cha kwanza kilichoanza dhidi ya Polisi kilikuwa na Ramadhani Kabwili,Mustafa Seleman,Gustava Saimon,Ally Ally,Kelvin Yondani,Abdulaziz Makame,Maybin Kalengo, Feisal Salum,David Molinga na Deus Kaseke.

Kocha huyo anayezungumzia Kiswahili cha lafudhi ya Kicongo amesisitiza kwamba anakifanyia mabadiliko makubwa kikosi hicho ili kupata ubora anaouhitaji tayari kwa mechi dhidi ya Township pamoja na ligi.

Amesema kuwa tangu kwenye mechi dhidi ya Kariobangi Jijini Dar es Salaam amekuwa akipangua kikosi na atafanya pia mabadiliko makubwa leo (jana) Jijini Arusha ingawa Spoti Xtra linajua kwamba kikosi cha leo ndio kitakachoanza dhidi ya Township.

Katika mazoezi ya jana (juzi) Jumamosi wachezaji waliofanya ni wale waliocheza mechi dhidi ya Polisi huku wengine wakipumzishwa hotelini, hiyo inamaanisha kwamba ndiyo watakaoanza mechi ya leo ingawa Yondani huenda akaongezwa.

“Kwenye hizi mechi za kirafiki sichezeshi kikosi kamili, ndio maana hata tukipoteza sioni kama ni tatizo sana.

“Kinachotakiwa ni wachezaji kuonyesha uwezo wao kwenye mechi hizo, kama huwezi kunionyesha uwezo katika mechi za kirafiki utaonyesha wapi? Kwa kupata nafasi kwenye kikosi cha Yanga mwaka huu unapaswa kuonyesha utofauti mkubwa, ushindani ni mkubwa,”alisisitiza Zahera.

Post a Comment

0 Comments