Na Lydia Churi- Mahakama Njombe
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo ameanza ziara ya kikazi katika mikoa ya Iringa na Njombe na kutaka kuwepo kwa matumizi ya vipimo vya vinasaba (DNA) katika kesi za mauaji, ubakaji na unajisi kwa watoto ili kurahisisha uendeshaji wa kesi hizo na kusaidia haki kupatikana kwa wakati.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka alipomtembelea ofisini kwake, Jaji Mkuu amesema matumizi ya vipimo vya DNA katika kesi yatasaidia haki kupatikana ambapo aliyetenda kosa atatiwa hatiani na asiyetenda kosa ataachiwa mapema.
“Kipimo cha DNA husaidia kuthibitisha kosa lililofanyika lakini bahati mbaya, kwa uzoefu wetu hatuoni matumizi ya kipimo hicho”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema kutokutumika kwa kipimo cha DNA Mahakamani, mshtakiwa huweza kuachiwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi.
“Eneo hili tumeona huweza kusababisha mtuhumiwa kuachiwa huru kwa sababu sisi tunaangallia zaidi ushahidi” alisisitiza Jaji Mkuu.
Alisema wakati mwingine Jaji au Hakimu huweza kuona wazi kuwa mshtakiwa alistahili kutiwa hatiani lakini ushahidi unapokosa uzito mtuhumiwa huachiwa huru.
Akifafanua, Jaji Mkuu Alisema kesi kama hizi huchukua muda mrefu na kusababisha wakati mwingine ushahidi muhimu kufifia kiasi kwamba kesi inapofika mahakamani lile joto la ushahidi lililoonekana wakati wa tukio huweza kupotea.
Alisema kutokana na kukua kwa sayansi na Teknolojia hivi sasa hatua kubwa imefikiwa katika matumizi ya kipimo cha DNA na kurahisisha sana. Akitolea mfano wa kesi ya ubakaji au unajisi kwa watoto wadogo alisema badala ya kumuhoji mtoto mdogo mahakamani, kipimo hiki huweza kutumika ili kuthibitisha kosa lililofanyika.
Alisema Serikali kwa kushirikiana na Mahakama hawana budi kuifanyia kazi changamoto hii ili kila raia anayetenda kosa atiwe hatiani na asiye na kosa aachiwe huru mapema hata katika hatua ya upelelezi wa kesi husika.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu alisema suala la ujazaji wa fomu za taarifa ya Daktari yaani PF 3 halizingatiwi kwa kuwa fomu hizo hazijazwi kwa ufasaha na hivyo huweza kusababisha mtuhumiwa kuachiwa huru wakati mwingine.
“Fomu hii inayo maeneo muhimu ya kujazwa na hasa yanayohitaji vipimo na endapo itajazwa kwa ufasaha itasaidia sana katika kuhakikisha mtu anayetenda kosa anatiwa hatiani”, alisema.
Kuhusu kesi za Mirathi, Jaji Mkuu alisema eneo hili lina changamoto kwa kuwa kesi hizi pia huchukua muda mrefu zaidi hivyo elimu haina budi kutolewa hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini. Alisema wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa kila mtu anapaswa kujitahidi kutafuta chake badala ya kutegemea cha marehemu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe alimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kujitoa kwake katika kuhakikisha Mahakama inatoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi na pia alimpongeza kwa kuendeleza ushirikiano na Mihimili ya Serikali na Bunge.
Aidha, Mhe. Ole Sendeka ameahidi kushirikiana kwa karibu zaidi na Mahakama ya Tanzania inapotekeleza majukumu yake ya msingi ya utoaji wa haki kwa wakati.
Katika ziara iliyoanza leo, Jaji Mkuu ametembelea Mahakama ya wilaya ya Makete na kuzungumza na watumishi wa Mahakama hiyo lakini pia alipata nafasi ya kukagua ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Makete.
0 Comments