Katika kile kinachoonekana ni kama kuwa wagumu kibiashara, Klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa imeendelea kumuwekea ngumu staa wao Neymar kuondoka baada ya kukataa ofa ya Barcelona kwa mara nyingine.
Dirisha la usajili la Ulaya linatarajiwa kufungwa Jumatatu ya Septemba 2, ambapo sasa Barcelona wanafanya kazi kubwa kutaka kumrejesha Mbrazili huyo kwenye timu yao lakini hali ya mambo bado ni ngumu kwa kuwa PSG wanaonekana kuwa na masharti magumu.
Inaelezwa kuwa baada ya mazungumzo ya siku mbili baina ya wawakilishi wa klabu hizo, Barcelona walikuwa tayari kutoa pauni 118m pamoja na wachezaji wao wengine wawili Ivan Rakitic na Jean-Clair Todibo pamoja na kumtoa Ousmane Dembele kwa mkopo wa mwaka mmoja, lakini vyote vimekataliwa.
PSG wanaamini ofa hiyo ni ndogo licha ya kuwa mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya wazi ya kutaka kuondoka klabuni hapo, kwa kuwa wao wanataka kiasi cha zaidi ya pauni 198m ambacho wao walikitoa ili kumsajili Neymar miaka miwili iliyopita.
Inadaiwa kuwa PSG wao wanataka fedha kamili ile wanayo itaka wao na hawataki kipengele chochote cha kupunguza fedha za usajili ikiwa kuna lolote litatokea mbele.
Taarifa nyingine zinaeleza kuwa wapinzani wa jadi wa Barcelona ambao ni Real Madrid, wao wapo kwenye mazungumzo mazuri ya kufanikiwa kumsajili mchezaji huyo. Neymar hajaichezea timu yake ya sasa tangu kuanza kwa msimu huu kutokana na kuandamwa na majeraha ya kifundo cha mguu ambayo yalisababisha pia akakosa michuano ya Copa America 2019
0 Comments