Windows

DJ maarufu kutoka Sauz kutangaza Global Radio

Na Andrew Carlos

UKIFIKA nchini Afrika Kusini ‘Sauz’ kisha ukaulizia DJ’s wakali ni wazi utatajiwa DJ Tira, Black Coffee, DJ Oskido, DJ Fresh na DJ Sbu.

Lakini ukiuliza nani mkali zaidi yao jibu la kwanza kabisa litakuwa DJ SBU. Yes! DJ Sbu ambaye jina lake kamili ni Sbusiso Leope ni mmoja kati ya Ma-dj wakali Afrika Kusini kutoka katika Jiji la Johannesburg.

Taarifa ikufikie kuwa, DJ huyo maarufu ambaye pia ni bonge moja la prodyuza, mjasiriamali, mtangazaji, mhamasishaji wa kimataifa na tegemeo kubwa la vijana katika kutoa misaada mbalimbali, anatarajiwa kutua Dar siku ya Jumatatu na moja kwa moja kufika katika Studio za +255 Global Radio, Sinza-Mori.

Akiwa Global Radio, kwa mara ya kwanza DJ Sbu atapata wasaa wa kutangaza ‘live’ kupitia kipindi maalum jambo ambalo hajawahi kulifanya na kituo chochote cha radio nchini.

Burudani

Mbali na kuwa DJ maarufu, Sbu amejipatia umaarufu kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2000 aliposhirikiana na mume wa memba wa Kundi la Mafikizolo, Nhlanhla, TK Nciza kufungua lebo kubwa ya muziki ya TS Records ikiwa ni muunganiko wa majina yao.

Lebo hiyo ambayo ipo Afrika Kusini, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwainua wasanii akiwemo mwanamuziki wa kike ambaye anaongoza kwa mauzo, Zahara.

DJ huyu yumo pia katika mafanikio ya muziki wa Kwaito kutokana na kuwakubali wasanii wa nyimbo hizo na kuwasaidia katika kuucheza muziki wao na kuutangaza ndani na nje ya Afrika Kusini.

Pia kwa kushirikiana na kampuni ya Times Media Group ya nchini humo, Sbu amefungua radio kubwa ya mtandao ya Massiv Metro akiwa na vipindi kibao vya burudani huku yeye akisimama kama mtangazaji kupitia kipindi chake cha The DJ Sbu Breakfast kinachoruka kila siku asubuhi.

Ujasiriamali

Unakumbuka kile kinywaji cha MoFaya kilichojipatia umaarufu na kukiita cha msanii Alikiba? Basi DJ Sbu ndiye mmiliki wa kinywaji hicho kinachoongeza nguvu ‘energy drink’.

Wakati anazindua kampuni na kinywaji hicho kinachokuja kwa kasi Afrika, alitumia njia mbili za kuzindua na kuuza ikiwemo kuuza mitaani kwa mtu mmoja mmoja pamoja na kuwatumia mastaa wakubwa Afrika kupiga nacho picha wakinywa.

Elimu

Katika elimu, DJ Sbu amekuwa akizunguka katika shule mbalimbali Afrika Kusini kutoa misaada ya kuwasomesha wanafunzi mbalimbali na kuwasaidia wale wenye mtatatizo ya akili kupitia taasisi yake ya Sbusiso Leope Education. Hadi sasa ameshatoa misaada ya kuwasomesha wanafunzi zaidi ya 500.

Uhamasishaji

Ukiweka pembeni hilo, Sbu ni mwandishi mzuri wa vitabu ambapo ana vitabu kadhaa kama Billionaires Under Construction ambacho hutumia katika majukwaa ya kuhamasisha.

Amekuwa akipata mialiko mingi ya kuhamasisha katika shule na vyuo mbalimbali kama Harvard Business School, Massachusetts Institute of Technology (MIT) na University of Westminster vyote vya Uingereza.

Jarida la Forbes Afrika limemuweka kama kijana wa Kiafrika wa kuangaliwa zaidi huku Gazeti la Sunday Times, Mail na Guardian yakimtaja mmoja kati ya vijana 200 shupavu wajao.

Sbu amepata shavu pia katika kituo kikubwa cha TV Afrika cha CNBC ambapo ana kipindi kiitwacho Kicking Doors with Sbu Leope ambacho kinaelezea ujasiriamali na vipaji kwa vijana.

Namna ya kuipata Global Radio ingia www.globalradio.co.tz au ingia kwenye playstore katika simu yako ya mkononi na andika 255 Global Radio.

The post DJ maarufu kutoka Sauz kutangaza Global Radio appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments