Na Saleh Ally
KABLA ya kuanza kwa msimu mpya wa mwaka 2019/20, Simba ilifanya usajili wa gharama kubwa unaokadiliwa kuzidi kitita cha Sh milioni 500 katika kuhakikisha inaimarisha kikosi chake.
Lengo namba moja la Simba lilikuwa ni kuvuka hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika kwa kuwa msimu uliopita, kikosi hicho kiliishia katika hatua hiyo.
Katika usajili, moja ya maingizo mapya kwa ajili ya kuimarisha kikosi hicho, Simba ilisajili viungo wawili ambao walicheza michuano ya Afrika katika nyanja kadhaa ikiwemo michuano ya Afcon nchini Misri.
Francis Kahata kutoka Gor Mahia ya Kenya ambaye alikuwa Misri wakati wa Afcon lakini kiungo mzoefu wa Sudan, Sharaf Shiboub ambaye amecheza mechi nyingi za Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na kigogo Al Hilal.
Simba walikuwa wakitangaza mara kadhaa, kwamba wanataka kwenda mbali Afrika na usajili wao unaangalia Afrika.
Katika kuimarisha kikosi, walisajili pia wachezaji watatu kutoka Brazil. Hawa ni beki Tairone Santos da Silva kutoka Atletico Cearense FC, kiungo na beki pia, Gerson Fraga Vieira na pia mshambuliaji Wilker Henrique.
Ilielezwa lengo la hawa ni usajili ambao unalenga kucheza Afrika ingawa ukiangalia kwa ndani zaidi unaona haya hayakuwa mapendekezo ya Kocha Patrick Aussems ambaye leo wengi wanaweza kumuona amekosea.
Usajili wa Wabrazili hawa, ilikuwa ni sehemu ya mabadiliko mapya ya Simba ambayo iliamua kujiimarisha zaidi huku ikiachana na nyota wake, Emmanuel Okwi ambaye zilielezwa sababu mbili, kwamba alikuwa msumbufu na baadaye kwamba alitaka fedha nyingi.
Simba huenda iliamua kuachana na usumbufu wa Okwi na kupiga hatua mbele ikiangalia kile ambacho inaamini ni sahihi kwa ajili ya maendeleo yake. Au fedha alizosema Okwi ili kuongeza mkataba zikaonekana ni nyingi, lakini uongozi ukaona bora kumwaga mkwanja mwingi kwa Wabrazili bao ambao hadi sasa, hawajaonyesha lolote.
Awali, nimesema halikuwa chaguo la kocha Aussems kwa kuwa wakati Simba inatolewa wachezaji hao hawakuwa wametumika katika michezo ya kimataifa.
Maana yake, Kocha Aussems hakuwa anawakubali au bado hajafurahishwa na kiwango chao ukiachana na mmoja, Wilker ambaye tulielezwa kuwa ni majeruhi.
Angalia, Simba imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya UD Songo na kuacha michuano ya Afrika. Vieira alikuwa katika benchi, alikuwa mmoja wa wachezaji ambao hawakuingia na unaona kwa mara nyingine tena kocha Aussems hakumtumia.
Angekuwa anamuamini sana, maana yake wakati akifanya mabadiliko ya kumpumzisha Kahata au Shiboub, basi bila shaka angemuingiza Vieira kuongeza nguvu na kuikoa Simba.
Simba inaangamia, Vieira alikuwa katika benchi na hakuwa katika nafasi ya kuingia kuikoa Simba kwa kuwa hakuonekana ni msaada.
Mbrazili mwenzake Wilker ni majeruhi lakini Dos Santos ameonekana bado hana kiwango bora cha kuwang’oa katika first eleven Erasto Nyoni au Pascal Wawa ambaye bado mashabiki wengi wasiojua mpira wanamtengenezea dharau licha ya kazi yake nzuri.
Simba imeachana na Juuko Murshid, hili lilikuwa jambo sahihi kwa kuwa Juuko alitaka kucheza anavyotaka au wakati anaotaka yeye. Lakini dos Santos au Vieira, wameonekana kushindwa kuvaa viatu hivyo.
Kwa kuwa ni wachezaji bora kutoka Brazil, nchi inayoaminika kuwa na wachezaji bora kabisa, bila shaka walitakiwa kuwa msaada kwa Simba tokea mwanzo na si baadaye.
Kuna haja ya kujifunza, nimesema ninaamini Wabrazili hao hawakuwa chaguo la Kocha Aussems. Kam ni yes, basi iko haja ya kujifunza kwamba papara ya kuamini mawakala bila kumshirikisha kocha kwa asilimia 100 ni tatizo kubwa sana.
Kama itakuwa ni kocha kweli amewataka, basi pia kutakuwa na tatizo kwa kuwa ameshindwa kuwatumia akionyesha hawaamini na tumeona wamekuwa katika maandalizi ya Simba nchini Afrika Kusini na hapa nyumbani. Vipi wasiwe tayari kuisaidia Simba?
Ukisema ukweli unawaudhi watu, lakini ukweli ni dawa na bora wanaochukia wafanye hivyo lakini taarifa ya kile walichoboronga kiwafikie.
Ninaamini walikuwa na nia nzuri lakini huenda walikosea kwa kuwa ilikuwa ni vigumu kuchukua ushirikiano. Kwenye klabu zetu wako wanaoamini wanajua kila kitu kumbe wana mengi wanapaswa kujifunza bila ya wao kujua kuwa inatakiwa kuwa hivyo.
Hauwezi ukawa Simba ukawa unajua kila kitu wakati walio Manchester United, Barcelona na klabu nyingine kubwa duniani wanaendelea kujifunza kwa mifano na yanayotokea. Vizuri kukubali kufundishwa ili kuongeza ujuzi wa ulichonacho.
Mfano, baada ya Simba kung’olewa na UD Songo nilijaribu kutengeneza utafakari katika mambo kadhaa ili kuangalia utamu wa maumivu ya mafunzo wanayoyapata viongozi.
Ninaamini kwa yeyote angeweza kujiuliza, kipi kilikuwa ni bora kumbakiza Okwi au kuwasajili Wabrazili ambao wamejiunga na Simba na kukaa nje, wakati Okwi angeweza kuwa msaada kuhakikisha Simba inabaki kwa kuwang’oa UD Songo.
Okwi alikuwa na shetani msumbufu, lakini leo malaika wake ametuonyesha ni bora kuliko shetani wa Wabrazili ambao malaika wao hadi leo hajaonyesha msaada kwa Simba.
Alichotaka Okwi, kingekuwa ni nyongeza lakini bado Simba ilikuwa ikimhitaji, kigezo cha usumbufu wake ambaye ni shetani wake, hakikuwahi kumzuia malaika wake ambaye ni msaada kwa Simba asitanue mabawa yake.
Kawaida, Simba watawekeza nguvu kwenye Ligi Kuu Bara. Mwanzo wa mafunzo kupitia Wabrazili utakuwa huu, kama wataweza kupambana basi itakuwa ni tatizo la kuwachelewesha lakini wakishindwa, litakuwa funzo jipya na usajili lazima kocha ashirikishwe kwa ukaribu na usajili uwe na umakini wa hali ya juu kwa kuangalia kikosi na mazingira sahihi ya nchi au bara kwa kuwa Tanzania, si Brazil na Afrika si Amerika Kusini.
0 Comments