SIMBA imekataa ofa ya dau la dola 300,000 (zaidi ya shilingi milioni 688) kutoka moja ya klabu ya nchini Saudi Arabia, iliyokuwa inamhitaji mshambuliaji wao, John Bocco.
Bocco ambaye ni nahodha wa timu hiyo, hivi karibuni aliongezewa mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kuichezea Simba kwa dau la shilingi milioni 100. Mshambuliaji huyo aliongeza mkataba huo ikiwa ni siku chache baada ya kukataa ofa kutoka Bidvest Wits inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini huku tetesi zikidai alisaini mkataba wa awali.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, Bocco alikuwa tayari kujiunga na timu hiyo ya Saudi Arabia, lakini Kocha Mkuu, Mbelgiji, Patrick Aussems alizuia kumuachia mshambuliaji huyo. Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kocha huyo alikataa kumuachia mshambuliaji huyo kwa sharti la kutafuta straika mwingine wa aina yake kwenye usajili wa dirisha dogo, ndiyo amuachie.
“Ilikuwa ngumu kwa kocha kukubali kumuachia Bocco aondoke Simba, kwani tofauti na Kagere hakuna mshambuliaji mwingine mwenye uwezo, licha ya kusajiliwa straika Mbrazili. “Hivyo, kocha amewakatalia viongozi kumuuza Bocco licha ya dau kubwa la usajili walilowekewa mezani.
“Hivyo, Bocco ataendelea kubakia Simba labda dirisha dogo viongozi watakaposajili washambuliaji wengine watakaochukua nafasi yake ndiyo na yeye aondoke,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa katibu wa timu hiyo, Dk Arnold Kashembe kuzungumzia hilo alisema: “Hilo suala bado halijafika mezani kwangu, hivyo ngumu kulizungumzia kwa hivi sasa (anacheka). Kuwa na subira.”
The post Bocco apata dili la mil 688 Saudi Arabia appeared first on Global Publishers.
0 Comments