Windows

Waziri Mkuu akagua maandalizi ya Terminal III


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua jengo la tatu la abiria kwenye kiwanja cha ndege cha Mwalimu Nyerere ili kuona maandilizi ya mapokezi kwa wajumbe wa mkutano wa SADC.

Akizungumza na watendaji wa Serikali pamoja na Kamati ya maandalizi uwanjani hapo Jumatano jioni, Waziri Mkuu amesema maandalizi ni mazuri isipokuwa kwa kasoro chache zilizobakia.

“Nimepita VIP hakuna shida. Pale terminal 2, sehemu ya Uhamiaji iko vizuri, uchunguzi wa afya nayo iko vizuri, lakini vyoo inabidi vibadilishwe haraka sana. Vile vyoo pale nje vimechoka, vibadilishwe mara moja, siyo tu kwa ajili ya ugeni, bali ni kwa faida yetu pia,” amesema huku akimwagiza meneja wa uwanja huo, Bw. Paul Lugasha aharakishe zoezi hilo.

Katika jengo la tatu la abiria kwenye uwanja huo, Waziri Mkuu amekagua eneo ambalo viongozi wakuu wa nchi watashukia, watakagua gwaride la heshima na kuangalia vikundi vya ngoma. Pia amekagua vyumba ambavyo watapumzikia kabla ya kuelekea mjini.

Amesisitiza kuwa usafi wa barabarani bado hauridhishi sababu kuna mawe, udongo na michanga kwenye barabara kuu ya kutoka uwanja wa ndege hadi mjini. “Tulikubaliana kuwa zile bustani ziboreshwe, vyuma vya barabarani vitengenezwe lakini hata leo nimepita kwenye fly-over, bado kuna mawe na michanga, hata sijui vinatokea wapi,” alisema.

Amewataka wahusika waweke banners za kutosha za aina mbalimbali na picha za wanyama kutani, uwanjani hapo ili kuonesha kwamba kuna mkutano mkubwa unafanyika hapa nchini.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka Watanzania watumie fursa ya uwepo wa mkutano huo mkubwa kuendesha biashara zao na ujasiriamali.

“Ziko fursa nyingi za uwepo wa mkutano huu. Kila mmoja atumie nafasi hii kuweza kuongeza na kuboresha kazi yake inayomletea uchumi,” amesema.

Post a Comment

0 Comments