Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia Taifa la Uganda ni mojawapo ya mataifa ambayo yalipokea pesa nyingi kutoka nje mwaka wa 2018.

 Uganda ilikuwa ya pili na ya sita kwa ukubwa kupokea pesa kutoka kwa mataifa mengine katika ukanda wa Afrika Mashariki na kusini mwa Sahara.

Kulingana na ripoti hiyo, mataifa ya Nigeria, Ghana, Kenya, Senegal, Zimbabwe na DR Congo pia yalipokea pesa nyingi kutoka kwa mataifa ya ughaibuni kushinda mataifa mengine.

Uganda ilipokea dola bilioni 1.2, Nigeria dola bilioni 24.3, Ghana dola bilioni 3.8 na Kenya dola bilioni 2.7. Senegal ilipata dola bilioni 2.2, Zimbabwe ikapata dola bilioni 1.9 na DR Congo ikapata dola bilioni 1.4 mwaka 2018. Kipato cha Uganda kiliongezeka kutoka dola bilioni 1.1 mwaka wa 2017, na kuchangia kwa ukuaji wa pato la kitaifa kwa takriban asilimia 4.5.

Awali ripoti ya Benki ya Dunia ilionyesha kwamba kipato kikubwa cha Uganda kinatoka mataifa ya mashariki ya kati, ambako Uganda inajivunia kuwa na wafanyikazi wake takriban 150,000.