Windows

Naibu Waziri Masauni akerwa na aliyoyaona kwenye magereza


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad  Masauni, amesikitishwa jinsi mahabusu na wafungwa walivyojaa katika magereza akidai wengine wapo humo kutokana na kuonewa.

Kutokana na hali hiyo aliagiza wakuu wa magereza nchini, makamanda wa polisi, kamati za kuharakisha kesi na watumishi wengine wa wizara hiyo, kuanza kuwasikiliza mahabusu na wafungwa katika magereza yote nchini na kupitia upya sababu zilizowafanya kuwekwa magerezani.

Agizo hilo alilitoa jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya majumuisho ya ziara yake katika mikoa ya Tabora, Geita na Mwanza.

Katika ziara hiyo, alitembelea magereza mbalimbali likiwamo la Butimba na kuwasikiliza wafungwa na mahabusu ambapo alisema ameshuhudia na kuelezwa mambo ya ajabu.

Masauni alisema  akiwa Mkoa wa Tabora alikutana na mwanamke aliye na mtoto na amewekwa mahabusu  miezi mitano bila kupelekwa mahakamani  jambo ambali alisema si la kiungwana.

“Suala la magereza kujaa hili ni tatizo sugu hapa nchini lakini nimepata picha fulani baada ya kutembelea magereza ya Tabora, Geita na leo (jana) nipo Mwanza katika gereza kuu la Butimba, niwaambie kabisa bila kificho huu msongamano tunaosema kila siku  kwa asilimia kubwa sisi viongozi  hasa wakuu wa magereza, makamanda wa polisi na zile kamati za kuharakisha kesi, hamfanyi kazi zenu.

“Hii tabia ya kusubiria mpaka viongozi wa kitaifa tuje mikoani kuwaelekeza cha kufanya katika maeneo mnayoongoza naomba mbadilike, nasema muda wenu wa kushikilia nafasi zeni upo katika matazamio kama hamtawajibika kwa kujiwekea malengo.

Hata hivyo Masauni alimtaka Mkuu wa  Gereza  la Butimba, Hamza  Rajabu kumweleza anavyotekeleza sera ya Serikali ya viwanda ambapo alisema ndani ya gereza hilo kuna kiwanda cha ushonaji nguo na wamekuwa wakipata kazi mbalimbali kutoka wa mashirika ya umma na binafsi.



Post a Comment

0 Comments