UONGOZI wa Yanga hivi karibuni umemkabidhi mshambuliaji wake raia wa Namibia, Sadney Urikhob jezi namba 17 ambayo ilikuwa ikivaliwa na Mrundi, Amissi Tambwe.
Kutokana na rekodi mbambali ambazo Tambwe amefanikiwa kuziandika akiwa na kikosi cha Yanga huku akiwa amevalia jezi hiyo, unaweza kusema kuwa Sadney amepewa mtihani mzito wa uongozi huo kwani atahitajika kufanya mambo makubwa uwanjani kama yale ambayo alikuwa akiyafanya Tambwe akiwa amevalia jezi hiyo.
Baadhi ya rekodi ambazo Tambwe alifanikiwa kuziandika ndani ya Yanga akiwa amevalia jezi namba 17 ni pamoja na ile ya kuibuka mfungaji bora msimu wa 2015/16 ambapo alifanikiwa kufunga mabao 21.
Lakini pia Tambwe ndiye mchezaji wa kigeni katika kikosi cha Yanga anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko wengine wote waliowahi kuitumikia timu hiyo kwa muda wote.
Tangu msimu wa 2014/15 akitokea Simba mpaka msimu wa 2018/19 amefanikiwa kuifungia Yanga mabao 52 katika michuano ya ligi kuu pekee, ambapo msimu wake wa kwanza alifunga mabao 13, msimu wa pili akafunga mabao 21, msimu wa tatu akafunga mabao 10, msimu uliofuata hakufunga bao lolote kutokana na kutumia muda mwingi akiwa nje ya uwanja akiuguza majeraha ya goti, lakini msimu uliopita alifanikiwa kuifungia timu hiyo mabao nane.
Rekodi nyingine ambayo Tambwe anaishikilia ni ya kuifunga Simba, akiwa na kikosi cha Yanga amefanikiwa kuifunga Simba mara mbili katika michuano ya ligi kuu akiwa amevaa jezi namba 17 mgongoni.
Kutokana na hali hiyo, Sadney amepewa kazi kubwa na uongozi wa Yanga. Hata hivyo, akizungumzia ishu hiyo, Tambwe alisema:
“Ni kweli kabisa jamaa amepewa mtihani mzito wa kulinda heshima ya jezi hiyo, sababu ligi ya Bongo ni ngumu sana.
“Ila binafsi jamaa namwamini sana, anajua kufunga, hivyo anaweza kuilinda heshima hiyo kama tu atajituma mazoezi ili aweze kuwa fiti lakini pia asipatwe na majeraha.
The post Mnamibia wa Yanga apewa mtihani mzito appeared first on Global Publishers.
0 Comments