Aliyekua Mwenyekiti wa Kijiji cha Izava Mkoani Dodoma kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Sokoine Mndewa amejiuzulu nafasi zake zote na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Sokoine amefikia hatua hiyo ya kujiuzulu kutokana na kile alichoeleza kwamba Ni kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Chadema pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli.
Kada huyo wa Chadema amejiunga rasmi na CCM mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM Wilaya ya Chamwino, Sostenes Tumbo, Gavana wa Tarafa ya Itiso, Remidius Mwema pamoja na ambao walimkaribisha na kumuahidi ushirikiano katika kuwatumikia wananchi.
" Niseme ukweli ninaombe mnipokee Mimi nimezaliwa katika familia ya CCM hivyo ni kama mtoto amerejea nyumbani, sioni haja ya kuendelea kuwa mpinzani ilihali Rais Magufuli anatekeleza yale yote ambayo wapinzani tumekua tukiyapigia kelele kwa muda mrefu.
" Kama ni miundombinu anajenga, elimu ameboresha tena haina malipo, vituo vya Afya vinajengwa Nchi nzima Mimi ni nani niendelee kupinga mambo mazuri kama haya? Hivyo kuanzia leo ninajiuzulu nafasi zangu zote ndani ya Chadema na ninaomba CCM ikiwapendeza mnipokee," amesema Sokoine.
Nae Gavana Remidius amempongeza Sokoine kwa uamuzi huo wa kujiunga na CCM kwani anaamini kutaongeza kasi ya kuwatumikia wananchi wa Tarafa ya Itiso na kutekeleza ilani ya CCM.
" Tunafahamu utendaji kazi wako, wewe ni kiongozi kijana ambaye wananchi walikuamini, CCM ina taratibu zake hivyo naombeni wana-CCM mumpokee kijana wetu bila maneno maneno, tumpe ushirikiano ili kweli ajione yupo kwenye Chama ambacho kinaongoza Nchi," amesema Katibu Muenezi wa CCM, Sostenes Tumbo.
0 Comments