YANGA wamemwambia Mwinyi Zahera kwamba timu yake imepata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa kuanzia mwezi Agosti akapagawa kwa furaha na kuwasisitiza lazima kieleweke.
Amewasisitiza mara mbilimbili wakamilishe orodha yake yote ya usajili fasta kwani anataka kufanya mambo makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa kurejesha hadhi ya Yanga.
Yanga imepata ofa ya kushiriki michuano ya kimataifa baada ya Tanzania kuongezewa timu kutokana na ufanisi wa Simba msimu uliopita.
Sasa Tanzania itakuwa na timu nne.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, msomi Fredrick Mwakalebela ameliambia Spoti Xtra kwamba wanatengeneza kikosi cha aina yake na hawaendi kushiriki bali kushindana na lazima kieleweke.
Ameongeza kwamba wamepania kufanya kitu cha maana ili kurejesha hadhi ya Yanga kimataifa na ikiwezekana Tanzania ipate pointi nyingi zaidi na kuongezewa timu kimataifa.
“Tumefurahi kuona Caf, imetuongezea nafasi za ushiriki jambo ambalo kwetu tunaona sasa kama itaongeza chachu lakini pia usajili tuliofanya ni babkubwa, usajili wetu kocha ameutengeneza vizuri.
“Na ametusisitiza kila mchezaji asaini mkataba wa miaka mitatu na kuendelea kwavile anawaamini na hajapendekeza mchezaji mzigo.
“Hata kama tusingepata nafasi hii bado mwakani tulikuwa na nafasi kubwa tu ya kushiriki hasa ukilinganisha viwango vya wachezaji tulionao, watu wanatakiwa watambue tu kuwa kocha wetu aliona mbali.
“Baada ya taarifa za CAF kutufi kia, tulimpigia Zahera akasisitiza tuwasainishe fasta Wachezaji wote muhimu wa kigeni na ndani ili tuendane na michuano hiyo, hivyo hadi sasa tumeshasajili wote muhimu.
“Mashabiki wasiwe na wasiwasi juu ya kikosi chetu, tumezingatia ubora mapema zaidi hivyo hakuna sehemu tutakapolegeza hasa katika michuano ya kimataifa, maana hata wachezaji wa ndani ambao kocha ameshawapendekeza hakuna ambaye hana sifa ya kucheza kimataifa,” alisema Mwakalebela ambaye ni kiongozi wa zamani wa TFF.
CAF wataja tarehe MECHI za kwanza za Simba na Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu zitachezwa wikiendi ya Agosti 10 na 11 Jijini Dar es Salaam.
Ni wikiendi hiyohiyo ambayo KMC na Azam zitakuwa zinapambana kwenye Kombe la Shirikisho. Marudiano ya mechi hizo ni Agosti 24 na 25.
Tanzania ndiyo nchi ya kwanza Afrika Mashariki kupewa nafasi ya kuingiza timu nne kwenye mashindano hayo ya kimataifa na safari wamechukua nafasi ya Ivory Coast ambayo timu zao hazikufanya vizuri msimu uliopita.
The post Yanga Yafumua kikosi CAF appeared first on Global Publishers.
0 Comments