Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewata kaviongozi wote na watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi wizara kuwajibika ipasavyo na kudumisha nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Amesema ili kufikia lengo na dhamira ya kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali ya 2019/2020 kwa ufanisi, viongozi hao wanatakiwa waendelee kuwasisitiza wananchi washiriki ipasavyo kulinda miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Septemba tatu mwaka huu.
Pia, Waziri Mkuu amezitaka mamlaka husika zishirikiane na wadau wengine katika kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kukomesha ukataji hovyo wa misitu, uchafuzi wa bahari, mito na maziwa na taka za plastiki ili kulinda mazingira asilia.
Akizungumzia kuhusu bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 33.11, kati yake sh. trilioni 20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63. “Aidha, sh. trilioni 12.25, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania pamoja na Washirika wa Maendeleo waiunge mkono Serikali katika kutekeleza vipaumbele vilivyowekwa kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 ili viweze kutoa mchango wa haraka katika maendeleo ya uchumi na ya watu.
0 Comments