Windows

Tshs. Bilioni 400 zatengwa kupeleka Umeme kwenye Maeneo haya


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetenga kiasi cha shilingi bilioni 400 kwa ajili ya kazi ya kusambaza umeme kwenye maeneo takribani 754 yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme lakini hayana umeme.

Hayo yalisemwa jana jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati wa Majumuisho ya Semina ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyohusu utekelelezaji wa miradi ya umeme vijijini na mradi wa Kinyerezi 1 Extension (MW 185).

Semina hiyo ya siku moja ilihudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt.Hamisi Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo, Menejimenti ya Wizara ya Nishati, REA na TANESCO.

“TANESCO imeshajipanga kufanya kazi hiyo na Wizara inaendelea kusimamia kazi hizi za usambazaji umeme ili kuhakikisha kuwa zinafanyika kwa ufanisi na tumeshafanya vikao mara kadhaa ili na wadau wanaohusika na usambazaji umeme wakiwemo Mameneja wa TANESCO nchi nzima lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme.” Alisema Naibu Waziri.

Aliongeza kuwa, katika mwaka wa Fedha unaoanza mwezi wa Saba mwaka huu, kipaumbele kitakuwa ni usambazaji umeme katika maeneo mbalimbali nchini kwani kila siku kuna ziada ya umeme ya kiasi cha megawati 250 hadi 300 kwa siku.

Aidha kuhusu usambazaji umeme katika Taasisi za umma kwenye miradi ya umeme vijijini alisema kuwa, Serikali kupitia REA na TANESCO itaweka kipaumbele cha kupeleka umeme kwenye maeneo hayo ili uwepo wa nishati kwenye vijiji hivyo uwe na tija.



Post a Comment

0 Comments