Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na Wakenya sanjari na kuwa watulivu wakati wakilifuatilia suala hilo kidiplomasia.
Kauli ya Waziri mkuu, imekuja kufuatia matamshi ya kibaguzi iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Starehe nchini Kenya Charles Njagua maarufu kwa jina la kisanii Jaguar ambaye kupitia kipande chake cha video alisema "Watanzania na Waganda wanaofanya biashara Kenya, hatuwataki,tunawapa masaa 24 waondoke, wasipoondoka tutawapiga na hatuogopi mtu."
Hata hivyo kupitia ukurasa wake wa Twitter, Jaguar amesema kauli aliyoitoa haikumaanisha wakazi wa ukanda bali aliwalenga Wachina ambao wamevamia biashara zao, kauli inayokinzana na kilichopo katika viedo yake.
Awali Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwataka wabunge kutoa maoni yao kuhusu kauli hiyo ya kichochezi na kibaguzi na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wabunge akiwemo Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe.
Wabunge hao wengi wao waliitaka serikali kutokaa kimya na kuiagiza serikali kulifuatilia suala hilo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki suala ambalo limeshachukuliwa hatua sanjari na wengine kudai siyo la kulipuuza bali ni la kuitaka Serikali ya Kenya kuomba radhi na kukanusha.
0 Comments