Kuanzia Julai mosi mwaka huu serikali inatarajia kutoa tamko rasmi, litakalolenga kuhakikisha kila dereva wa lori na basi nchini, anakuwa na mkataba wake wa ajira.
Aidha, tamko hilo litalenga kuhakikisha wamiliki wa mabasi na malori hayo nchini, wanafuata na kutekeleza sheria za kazi na ajira.
Hayo yalibainishwa bungeni Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Anthony Mavunde wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema).
Katika swali lake la nyongeza, mbunge huyo alitaka kujua serikali inachukua hatua gani kushughulikia malalamiko ya madereva wa malori na mabasi, ambao takribani asilimia 90 hawana mikataba ya ajira. Sisi wa kule mipakani ndio tuna hali mbaya kila siku tunasikia migogoro baina ya madereva hawa na wamiliki kuhusu mikataba, serikali ina mpango gani kuharakisha jambo hili?Alihoji.
Mavunde akijibu swali hilo, alisema katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa mwaka 2015 wakati wa kampeni juu ya mikataba ya ajira, tayari wameanza kushughulikia suala hilo.
Alifafanua kuwa awali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), katika kutatua tatizo hilo, iliweka masharti kwa wamiliki wa magari hayo wanaoenda kuomba leseni, lazima maombi yao yaambatanishwe na mikataba ya ajira kwa ajili ya madereva wao.
"Hata hivyo, tuliona sharti hili bado lina walakini, sasa siku mbili zijazo yaani kuanzia Julai Mosi mwaka huu wizara itatema cheche kwani tutatoa tamko juu ya hatua gani zitachukuliwa kwa wamiliki wasiowapatia mikataba madereva wao lakini pia kuhakikisha kila dereva wa lori au basi anakuwa na mkataba wake wa ajira, alisisitiza Mavunde.
Alisema tamko hilo litatolewa kwa mtengamano wa wizara mbili, ikiwemo wizara hiyo ya ajira chini ya Jenista Mhagama na Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi chini ya Kangi Lugola.
0 Comments