JUZI Jumamosi inadaiwa kuwa viongozi wa Simba hawakuamini kile walichokiona kutoka kwa beki wao wa kati Mganda, Juuko Murshid alipokuwa akiitumikia timu yake ya taifa ya Uganda dhidi ya DR Congo katika michuano ya AFCON inayoendelea nchini Misri.

 

Uwezo wa juu aliounyesha Juuko katika mchezo huo na kuiwezesha Uganda kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ndiyo hasa uliyowavuruga viongozi hao na kujikuta wakijutia maamuzi yao
ambapo inadaiwa kuwa tayari wameyachukua dhidi ya beki huyo.

 

Inadaiwa kuwa baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, hivi karibuni, uongozi wa Simba ulipanga kuachana na Juuko kutokana na kile kinachodaiwa ni kutoridhishwa na uwezo wake uwanjani jambo ambalo limeufanya uongozi huo hivi sasa kuwa katika harakati za kusaka mbadala wake.

Akizungumza na Championi Jumatatu, mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe gazeti alisema kuwa kiwango alichonyesha Juuko juzi uwanja dhidi DR Congo kimewacha viongozi hao wasijue la kufanya dhidi yake.

“Juuko katuonyesha kuwa bado ni mchezaji muhimu sana katika kikosi chetu, sijui uongozi wa juu unaosimamia usajili utaamua nini kwa sababu walikuwa tayari na mpango wa kuachana naye kutokana na madai ya kutoridhishwa na uwezo wake.

 

“Lakini sasa ametuonyesha kuwa uwezo wake upo juu tofauti na tunavyofikiria na jana kusema kweli wengi wetu tumetofautiana kimtazamo kwa sababu yake,” alisema kiongozi huyo.

 

Hata hivyo, nahodha wa zamani wa Simba, Selemani Matola ambaye sasa ni kocha wa Polisi Tanzania amelizungumzia hilo kwa kusema kuwa anawashauri viongozi Simba kufikiri juu ya maamuzi yao wanayodaiwa kuyachukua dhidi ya Juuko.

 

“Juuko bado ni mchezaji muhimu sana katika kikosi cha Simba, hali ya kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Uganda inatosha kabisa kuwaambia kuwa si mchezaji wa kiwango cha chini. “Kila mtu ameona uwezo wake jinsi gani alivyo msaada kwa timu yake taifa, Simba kama wanataka kumuacha basi labda wamwachie kwa sababu nyingine ila siyo uwezo,” alisema Matola

The post Juuko Awavuruga Viongozi Simba appeared first on Global Publishers.