Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema kazi ya uchambuzi wa taarifa za utafiti wa mafuta na gesi uliofanywa na kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah, inatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Alisema katika mchakato huo, wataalamu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wanashiriki.
Alikuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha 2019/2020 katika kikao cha bajeti kinachoendelea katika ukumbi wa baraza la wawakilishi, Chukwani.
Aidha alisema, serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, imeandaa rasimu tatu za kanuni ambazo ni kanuni ya uchimbaji, kanuni ya ada na vibali na kanuni ya uwasilishaji wa taarifa za kila siku.
Alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Gesi (ZPRA) imejiandaa kufanya mazungumzo na kampuni nyengine zitakazohitaji kuwekeza katika sekta ya utafutaji wa mafuta na gesi baada ya kukamilika kwa hatua ya kuvigawa vitalu vyengine vilivyopo Zanzibar.
Kuhusu pato la taifa, alisema kwa mwaka 2019 linatarajiwa kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.8 itakayosababisha kuimarika zaidi kwa uchumi kutokana na ongezeko la uwekezaji katika sekta ndogo ya usafirishaji na uvuvi.
Alisema hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa pato la mwananchi kutoka shilingi milioni 2.1 sawa na dola za Marekani 944 na kufikia shilingi milioni 2.3 sawa na dola 1,026.
Alisema Zanzibar tayari imekaribia kufikia kiwango cha nchi ya kipato cha kati cha dola za Marekani 1,030 kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa.
Alisema pato la taifa kwa bei ya soko limefikia thamani ya shilingi 3.663 bilioni kwa mwaka wa fedha 2018 kutoka thamani ya shilingi bilioni 3.228 kwa mwaka 2017 kulikosababishwa na ongezeko la pato la mwananchi.
Alisema kasi ya mfumko wa bei pia imeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2017 baada ya kuchukuliwa hatua za kuudhibiti.
Alieleza kwamba muelekeo wa hali ya uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2019 unategemewa kwenda sambamba na utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2020, mkakati wa kukuza uchumi Zanzibar (MKUZA III) na ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.
Alisema mafanikio yote yaliyopatikana yanatokana na jitihada zinazochukuliwa na serikali chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein.
Alisema azma ya serikali ni kuhakikisha inakamilisha miradi yote mikubwa ya maendeleo kama ilivyoahidi katika ilani ya uchaguzi ya chama ya mwaka 2015/2020.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa jengo la abiria (terminal 3) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume, ujenzi wa bandari ya Mpiga Duri Maruhubi na Ujenzi wa hospitali Binguni.
Alisema miradi hiyo inakwenda sambamba na mpango wa taifa wa kuendelea kuimarisha uzalishaji na usafirishaji wa zao la karafuu kutokana na matarajio ya msimu mkubwa wa zao hilo kwa mwaka 2019 pamoja na kupanuka kiwango cha idadi ya watalii kutokana na kupatikana kwa masoko mapya ya sekta hiyo.
Alisema kwamba serikali tayari imeandaa mikakati ya kutafuta fedha kwa nchi na mashirika rafiki sambamba na kutenga fedha kutoka katika vianzio vyake vya ndani ikiwa itapotokezea kushindwa kupata msaada kutoka nje serikali iendelee na ukamilishaji wa ujenzi wa miradi hiyo.
0 Comments