


WAKIWA wamebakiwa na mechi mbili mkononi, uongozi wa Yanga unaamini kuwa timu yao bado ina nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa sababu watani zao Simba "pumzi" yao imekata.
Mechi mbili za Yanga zilizobakia msimu huu ni dhidi ya Mbeya City inayotarajiwa kuchezwa Jumatano na ile ya kufunga msimu huu kwa kukutana na Azam FC, mechi zote kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, aliliambia gazeti hili kuwa wanachama na mashabiki wa timu yao wanatakiwa kuwa watulivu kwa sababu kwenye soka lolote linaweza kutokea.
Mwakalebela alisema kuwa licha ya watani zao kuwa na mechi nyingi mkononi, bado hiyo haina maana wanaweza kupata ushindi katika michezo yote.
"Bado hatujakata tamaa, kikubwa tunatakiwa kushinda mechi zetu mbili zilizobaki, mpira ni mchezo wa makosa, lolote linaweza kutokea kwa Simba na hatimaye tukafanikiwa kupata ubingwa," alisema Mwakalebela, Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mabingwa watetezi, Simba ambao wamecheza mechi 34, wamebakiza michezo dhidi ya Ndanda FC, Singida United, Biashara United na Mtibwa Sugar.



0 Comments