STRAIKA kinara wa mabao wa Yanga, Heritier Makambo ametua rasmi Horoya AC ya Guinea kwa mkataba wa miaka mitatu, ikiwa ni miezi michache tangu asaini Jangwani.
Usajili wa Makambo kwa klabu hiyo ya nje, iliripotiwa mapema wiki iliyopita na Gazeti hili baada ya kupenyezewa na juzi Alhamisi Mkongoman huyo alisaini mkataba huo wa kuichezea timu hiyo ambayo ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Makambo ameondoka Yanga akiiacha timu hiyo ikichuana na Simba kwenye mbio za ubingwa kwani, mabao yake 16 yaliisaidia kuongeza chachu katika ligi hiyo, huku akichuana na nyota wa timu nyingine katika kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji.
Kuondoka kwa Makambo akiwa ameichezea Yanga kwa muda mfupi ni muendelezo wa nyota wa kigeni wanaokuja Tanzania kama njia yao ya kupata maisha ya neema katika mataifa mengine. Ipo orodha kadhaa tangu kipindi kile cha Shaaban Nonda ‘Papii’ ambaye aliichezea Yanga kwa kipindi kifupi miaka ya katikati 1990 baada ya kumpokea kutoka Atletico Olympic ya Burundi alikozaliwa, japo anatambulika kama Mkongoman.
Hakuna asiyejua nyota huyo alivyochukuliwa poa nchini, lakini akaenda kuwa shujaa katika klabu alizozichezea kuanzia Vaal Professionals ya Afrika Kusini FC Zurich ya Uswisi, Rennes na Monaco za Ufarssna, AS Roma ya Italia na hata Blackburn Rovers ya England.
Kwanini tumeamua kuujadili usajili wa Makambo na kuujumuisha na nyota kadhaa wa kigeni waliowahi kucheza Tanzania kabla ya kutimka kwenye maaifa mengine?
Kuna utofauti mkubwa wa wachezaji wazawa na wale wa kigeni katika kutafuta maisha nje ya nchi zao na hili ndilo limetufanya kuwakumbuka akina Nonda na wenzao baada ya Makambo kutimka Yanga akiwa hata hajamaliza mkataba wake wa miaka miwili Jangwani.
Ukimuondoa Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Abdallah Hamis, David Naftar kwa kizazi hiki cha sasa ama kina Athuman Machuppa, Danny Mrwanda, Henry Joseph na Abdi Kassim ‘Babi’ wa enzi za nyuma ambao walikuwa wakitoka na kuingia hapa na pale, wachezaji wengi wa Tanzania ni waoga katika kujaribu maisha nje ya nchi yao.
Hivyo tulikuwa tunadhani, imefika wakati wachezaji wa Kitanzania kujaribu kujifunza kutoka kwa wenzao, kitu gani kinawafanya kuwa na mioyo ya kijasiri ya kukubali kusaka maisha nje ya mataifa yao bila kujali upweke ama changamoto watakazokutana nazo.
Makambo anafaa kuwa mfano kwa akina Ibrahim Ajibu, Feisal Salum, Gadiel Michael na nyota wa klabu nyingine katika kuchakarika kutafuta maisha nje ya Tanzania kwa vile wana vipaji vinavyoweza kuwafanya wacheze kokote kwa mafanikio makubwa.
Kina Samatta, Simon Msuva, Shiza Kichuya na wengine wanaocheza nje hata wao walikuwa waoga mwanzoni, lakini kule kujipa moyo na kuvaa ujasiri wa kutaka kucheza nje na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zimewafanya wafike hapo walipo.
Hivyo hata kina Ajibu, Said Ndemla, Jonas Mkude, Haruna Chanongo badala ya kufikiria usajili wa klabu za Simba, Yanga na Azam wafikirie zaidi kwenda nje kwa sababu sio tu itawasaidia kimasilahi, lakini itakuza akili zao kisoka kama ilivyo sasa kwa kina Samatta.
Samatta wa sasa ama Msuva wa sasa sio wale waliokuwa Simba na Yanga, wamepevuka na kuwa imara zaidi kwa sababu ya kukubali changamoto walizokutana nazo wakati walipoanza kucheza soka nje ya mipaka ya Tanzania.
Lakini kama wachezaji wazawa wataendelea kujiona hawawezi, wataendelea kuwa wa hapahapa na kupishana na fursa za kimaisha ya kuwakuza kiuchumi na kisoka na kuwaacha akina Makambo wengine wakija na kuondoka Tanzania wakiwaacha wakizeeka.
Wachezaji ni lazima watambue na kujua kuwa soka la kulipwa lina faida kubwa kwao na taifa kwa ujumla hasa inapokuja ushiriki wa michuano ya kimataifa kwa timu ya taifa, lakini pia thamani ya soko la mchezaji linabebwa zaidi na umri na kipaji.
Hivyo wachezaji wapambane kwenda nje ya nchi wakiwa na umri mdogo ili thamani yao iwe kubwa, badala ya kusubiri machweo ndipo wakurupuke kwenda na kisha kuishia kununuliwa kwa bei rahisi na pia kushindwa kulitumikia soka la kulipwa kwa muda mrefu. Ndio maana, tumeamua kuwakumbusha wachezaji wazawa, vijana na wenye vipaji kuwa, muda wa kuchakarika ni sasa kama alivyofanya Makambo.
0 Comments