Windows

Simba, Azam ni vita ya kibabe


leo Jumatatu nyasi za Uwanja za Uhuru jijini Dar es Salaam zitawaka moto zitakapokuwa zinawakutanisha Simba dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara huku Wekundu hao wa Msimbazi wakihitaji ushindi kwa namna yoyote ili kujiimarisha katika nafasi ya kutetea ubingwa huo.
Katika rekodi ya timu hizo ambazo makazi yao ni Dar es Salaam zimekutana mara 21 kwenye Ligi Kuu Bara tangu Azam FC ilipopanda msimu wa 2008-2009. Katika mechi hizo, Simba wameshinda michezo 10, Azam FC mmitano na wametoka sare mechi sita.
Katika mashindano yote, Simba imekutana na Azam FC mara 34, imeshinda mechi 16, Azam 12 na wametoka sare mara sita.
Kinara wa mabao katika michezo hiyo ni nahodha wa Simba, John Bocco ambaye amefunga magoli 20. Mabao hayo aliyafunga alipokuwa anaichezea Azam FC na baada ya kuhamia Simba anayoichezea mpaka sasa.
Kwa sasa vinara wa Ligi Kuu Bara ni Simba ambayo inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 81 baada ya kucheza mechi 32, Yanga wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 80 katika michezo 35 ambazo ni sawa na Azam FC iliyo ya tatu na pointi 68.
Mchezo wa Simba dhidi ya Azam ni miongoni mwa michezo iliyoshika hatma ya ubingwa wa Simba msimu huu, kwani wametoka kupoteza 1-0 kwa Kagera Sugar hivyo kwa namna yoyote wanahitaji ushindi ili kujiweka mahali pazuri.
Azam FC wao hawana cha kupoteza kwenye Ligi Kuu na akili yao, wameielekeza zaidi kwenye mchezo wa fainali wa Kombe la Shirikisho na watacheza na Lipuli FC.
Lakini, ngumu zaidi kwa Simba dhidi ya timu hiyo ya Bakhresa maarufu kwa jina la Wanalambalamba ni kutokubali kupoteza mara mbili mfululizo.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba waliibuka washindi kwa jumla ya mabao 3-1 mchezo ulipigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.



Post a Comment

0 Comments