Windows

Naibu Waziri Mavunde Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Mwakilishi Wa UNICEF Nchini

Na; Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa UNICEF nchini Bi. Maniza Zaman ambaye amemaliza muda wake alipomtembelea Ofisi kwake iliyopo Jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Mavunde amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF kwa kushirikiana na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo na kwa kutoa misaada katika sekta mbalimbali nchini.

“UNICEF imekuwa ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika masuala mbalimbali yaliyolenga kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii (Social Security Policy of 2003), kuwapatia mafunzo watumishi katika masuala ya virutubishi na hifadhi ya jamii, pia kuwapatia vitendea kazi kama vile komputa na magari ambayo yanatumika kwenye miradi mbalimbali,” alieleza Mavunde. 

Aliongeza kuwa, Serikali imeguswa na jitihada za UNICEF na itaendeleza ushirikiano na shirika hilo katika kutekeleza jukumu la kuhudumia Watoto.

Aidha, Naibu Waziri Mavunde alimpongeza Bi. Maniza Zaman kwa kazi nzuri aliyofanya kipindi cha muda wake na kumsihi kuendelea kuwa balozi mzuri wa masuala ya Watoto.

“Tutakukumbuka kwa juhudi na ushauri uliokuwa ukitupatia katika masuala ya elimu na haki za Watoto,” alisema Mavunde. 

Kwa upande wake, Bi. Maniza Zaman amesema anaishukuru Serikali kwa ushirikiano iliompatia kwa kipindi chote alichokuwa hapa nchini.
 



Post a Comment

0 Comments