Watu wawili wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kugongana na gari jingine mkoani Kilimanjaro.
Waliofariki ni Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Aanael Mbise (50) na Frank Macha (35) mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni fundi umeme.
Akizungumza leo Jumanne Mei 7, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo eneo la Kiverenge Wilaya ya Mwanga.
Issah amesema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota Prado iliyokuwa ikitokea Same kuelekea Moshi na basi dogo la kampuni ya KVC iliyokuwa ikitokea Moshi kuelekea Same.
"Kwenye ajali hiyo wamefariki watu wawili waliokuwa kwenye Prado, mmoja ni ofisa wa polisi mwenye cheo cha Mrakibu mwandamizi wa jeshi la Polisi na mtu mmoja amejeruhiwa na mwingine ametoka mzima," amesema
Amemtaja aliyejeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Samson Macha (23) ambaye ni Mkazi wa Dar es salaam na amevunjika mguu wa kushoto na anaendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Wilaya ya Same akisaidiwa na ndugu yake Daniel Macha.
Akielezea chanzo cha ajali hiyo Kamanda amesema,” Gari aina ya Toyota Prado ilihama upande wake na kuja kugongana upande na basi tunaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo."
Awali akielezea ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson amesema ajali hiyo ilikuwa mbaya na bado wanaendelea na uchunguzi ili kuweza kujua chanzo chake.
Na Florah Temba, Mwananchi
0 Comments