WAKATI Simba ikiendelea kupambana kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems amefunguka kuwa atahakikisha anafanya usajili mpya kwa lengo la kuweza kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika misimu ujao.
Aussems raia wa Ubelgiji ametoa kauli hiyo kufuatia mafanikio waliyopata kwenye msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufika Hatua ya Robo Fainali na kuondolewa na TP Mazembe ya DR Congo.
Kwa sasa Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 81 baada ya juzi Jumatano iliyopita kuibuka na ushindi wa mabao 8-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar huku Yanga ikiwa na pointi 80 kwenye nafasi ya pili.
Aussems alisema kuwa suala la kufanya usajili kwenye kikosi chake haliwezi kukwepeka kama kweli wanataka kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa msimu ujao na hilo lazima atalifanya.
“Nitafanya usajili kwa sababu najua malengo yetu ni kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao sasa suala la kuangalia wachezaji wapya kwa ajili ya kuongeza siwezi kulikwepa kama kweli tunataka tufike mbali,” alisema kocha huyo kauli ambayo inamaanisha kuwa ana imani kubwa timu yake itabeba ubingwa msimu huu katika ligi kuu.
“Unajua hii michuano iliyopita tumejifunza mambo mengi kutoka kwenye klabu kubwa ambazo zina uzoefu wa kutosha kuliko sisi, hata ukiangalia tumecheza robo fainali ila haiwezi kuwa kigezo cha kuona kwamba tupo imara lazima tuongeze watu ambao watakuwa na tija,” alisema Aussems na kuongeza:
“Nimepanga kuanza tathmini ya usajili kuanzia wiki ijayo, ambapo kwa sasa tunaangalia zaidi michezo yetu ya wiki hii ili tuone namna gani tutajiimarisha kileleni.”
0 Comments