ALIYEWAHI kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi uliopita wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Shija Richard, ameteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga.
Richard ambaye ni mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ni kati ya wajumbe wawili walioteuliwa na Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla, mwingine akiwa ni Athuman Kihamia ambao wataungana na wajumbe nane waliochaguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msolla, alisema amefanya uteuzi huo ili kuongeza idadi ya wajumbe ambao wataweza kuendana na kasi ya klabu hiyo wanayotaka kuiendesha kama taasisi kubwa.
Alisema licha ya kuteuwa wawili hao, bado kwa nafasi yake anaruhusiwa kuteua wajumbe zaidi, lengo ni kuongeza ufanisi katika utendaji.
“Tumeongeza wajumbe, lengo ni kuboresha eneo la utendaji, Shija na Kihamia wataungana na wajumbe nane waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita na pia nitaongeza wengine katika siku zijazo,” alisema Msolla.
Kwa upande wake, Kihamia ni miongoni mwa wanachama maarufu wa Yanga aliyewahi kushika nyadhifa ndani ya klabu mbalimbali nchini, kwa sasa akiwa ni mmoja wa vigogo wa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, Msolla alisema Jumamosi wiki hii watakuwa na hafla ya kuwafuturisha wachezaji wa timu hiyo kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Alisema katika hafla hiyo, wachezaji watapata nafasi ya kukutana na kamati nzima ya utendaji na wadau mbalimbali wa Yanga ili kuwatambulisha kwao kwa mara ya kwanza.
Msolla alisema siku hiyo walitaka kufanya tukio kubwa la uchangishaji kwa jijini Dar es Salaam, lakini wameahirisha hadi utakapomalizika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
0 Comments